LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 7, 2019

IRAN NA IRAQ ZAKARIBIA KUFUNGUA UKURASA MPYA WA USHIRIKIANO

Spika wa bunge la Iraq katika ziara yake hapa Tehran ameonana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kujadili kuimarisha ushirikiano kati ya pande mbili.
Mohammed al Halbusi Spika wa bunge la Iraq amefanya ziara nchini Iran katika hali ambayo irada ya viongozi wa nchi mbili hizi ni kuona ushirikiano kati ya Tehran na Baghdad unaimarishwa pakubwa. Iran na Iraq zikiwa nchi mbili jirani na zilizo na masuala mengi ya pamoja yakiwemo ya kiutamaduni na kidini zimekuwa zikichukua hatua za kuimarisha uhusiano kati yazo. Iraq ikiwa ni nchi jirani ina umuhimu mahsusi katika uhusiano wa nje wa Iran. Mtazamo wa Iran kwa Iraq ni mtazamo wa kistratejia na ndio maana usalama na amani ya Iraq ni usalama na amani ya Iran pia. Katika fremu ya mahusiano haya, wakati kundi la kigaidi la Daesh lilipoivamia Iraq na kuanza kuishambulia miji mbalimbali ya nchi hiyo; Iran ilitoa msaada wa haraka kwa Iraq katika fremu ya ushirikiano wa kistratejia wa pande mbili hizo na kulifurusha kundi la Daesh huko Iraq. 
Spika wa bunge la Iraq, Mohamed al Halbusi
Hivi sasa fursa mpya zimeandaliwa huko Iraq baada ya Daesh kusambaratishwa nchini humo ili Iran iendelea kuwa na nafasi chanya nchini humo kama nchi jirani inayoweza kuaminiwa na Iraq. Wakati huo huo mpaka mrefu na wa pamoja baina ya nchi mbili hizo, masuala ya kiutamaduni na kidini yanayowakutanisha pamoja wananchi wa Iraq na Iran na kufikia kwa urahisi masoko ya nchi hiyo na kuidhaminia mahitaji muhimu yote haya yametoa msukumo kwa nchi mbili hizi wa kuimarisha na kukuza ushirikiano kati ya pande mbili. 
Iran ikiwa nchi inayotegemewa na Iraq imeweza kuidhaminia nchi hiyo mahitaji yake muhimu katika sekta ya nishati. Misimamo ya wazi iliyodhihirishwa na Iraq na kutokubali kwake kuunga mkono vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran; imeipelekea Tehran na Baghdad kuazimia kufungua ukurasa mpya wa mashirikiano yao khususan katika sekta ya nishati. Katika fremu hiyo, tarehe 11 mwezi huu wa Machi Rais Hassan Rouhani wa Iran atafanya ziara huko Iraq. Ziara hiyo itakuwa ya kihistoria na nukta muhimu katika uhusiano wa Tehran na Baghdad baada ya kuundwa serikali mpya ya Iraq kwa kuzingatia hali ya mambo ilivyo katika eneo. Ziara ya Spika wa bunge la Iraq hapa Tehran na mashauriano ya kina aliyofanya na viongozi mbalimbali wa Iran ni utangulizi wa ziara ya kihistoria ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Iraq ili safari hiyo iweze kuwa na natija bora zaidi. 
Muhammad Javad Zarif waziri wa Mambo ya Nje wa Iran (katikati) katika mazungumzo na Mohammed al Halbusi Spika wa bunge la Iraq 
 
Akizungumza jana usiku na Spika wa bunge la Iraq, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: Irada ya kiuongozi, serikali na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ni kwa ajili ya kushirikiana kindugu na kwa karibu na Iraq.   
Iran na Iraq zina suhula na uwezo mkubwa katika upande wa kiuchumi kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi na kibiashara; na safari ijayo ya Rais wa Iran mjini Baghdad itaainisha ukurasa mpya katika uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili hizi. 
Kuhusiana na suala hilo, Reza Rahmani Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran aliashiria jana pambizoni mwa mazungumzo kati yake na Waziri wa Biashara wa Iraq hapa Tehran kuhusu uhusiano mzuri wa nchi mbili hizi na kusisitiza kuwa: Iran na Iraq zimeazimia kuongeza thamani ya mabadilishano yao ya kibiashara na kufikia dola bilioni 20 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.  
Iran ina nafasi nzuri ya kustawisha biashara na Iraq na kupanua uwezo wa kiuchumi wa nchi hiyo; masuala ambayo yana taathira chanya katika masuala ya pamoja ya kiutamaduni na kidini ya wananchi wa Iran na Iraq. Wakati huo huo fursa nzuri zimeandaliwa kwa kuzingatia mtazamo wa pamoja wa Iran na Iraq kuhusu umuhimu wa uhusiano wa nchi mbili hizi; ili kwa njia hiyo kuweza kuzidisha kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi mbili ambacho kwa sasa ni karibu dola bilioni 13 kwa mwaka na kufikia kile kilichokusudiwa yaani dola bilioni 20 kwa mwaka. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages