Rais wa Marekani, Donald Trump anaendeleza mashambulizi na vita vyake vya kibiashara dhidi ya mataifa mengine duniani kupitia kuziongezea ushuru bidhaa za kigeni zinazoingia Marekani na hivyo kusababisha vurugu kubwa katika miamala ya kibiashara ya kimataifa.
Ingawa hivi sasa makali ya upanga wa vita vya kibiashara vya serikali ya Trump yameelekezwa kwa China, lakini Marekani imeanzisha vita pia vya kibiashara na madola mengine makubwa ya kiuchumi kama Umoja wa Ulaya na pia dhidi ya mataifa yanayoinukia kiuchumi kama vile India na Uturuki.
Katika hatua ya karibuni kabisa, Trump amesema kuwa ataondoa vipaumbele vilivyopo hivi sasa kwa bidhaa za Uturuki na India akidai kuwa miamala hiyo ya kibiashara si ya kiadilifu. Siku ya Junatatu Trump aliwatumia barua spika wa Baraza la Congress na mkuu wa Baraza la Sanate la nchi hiyo akiwaeleza uamuzi wake wa kuziondoa India na Uturuki katika mpango wa GSP unaohusiana na kuondolewa ushuru bidhaa za baadhi ya nchi. Serikali ya Trump imesema kuwa, Washington ina nia ya kuzitoa India na Uturuki katika mpango huo wa Marekani kwani nchi hizo hazitimizi tena masharti ya kuwemo katika orodha ya GSP.
Maraifa wa Uturuki na Marekani
Serikali ya Trump imedai kuwa India imeweka vizuizi ambavyo vimeacha athari mbaya katika biashara ya Marekani. Amma kuhusiana na Uturuki, Washington imesema kuwa, nchi hiyo ambayo tangu mwaka 1975 imekuwa ikifaidika na mpango wa GSP, imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi na hilo lina maana kwamba haitimizi tena masharti ya kuwemo kwenye ratiba za GSP.
Uamuzi huo wa Marekani utaanza kutekelezwa takriban siku sitini tangu Trump alipe taarifa hiyo Baraza la Congress. Kwa mujibu wa mpango wa GSP, kama nchi itaweza kutimiza masharti kama vile kuiruhusu Marekani kutumia vizuri soko lake, basi nchi hiyo inaruhusiwa kuingiza Marekani baadhi ya bidhaa zake bila ya kudaiwa ushuru.
Anup Wadhawan, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa masuala ya kibiashara wa India amejibu vita hivyo vipya vya kibiashara vya Trump akisema kuwa, faida ambayo India ilikuwa inaipata kupitia mpango huo wa GSP si kubwa na ni kama dola milioni 190 tu, hivyo kutoka India kwenye mkataba huo hakutoathiri chochote.
Itakumbukwa kuwa, mashinikizo ya kiuchumi ya Trump dhidi ya Uturuki yalianza mwezi Agosti 2018. Wakati huo kulizuka mivutao mkubwa ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili kuhusiana na kasisi wa Kimarekani, Andrew Brunson ambaye alitiwa mbaroni na Uturuki kwa tuhuma za kushirikiana na genge la kigaidi la PKK. Hivyo Trump alichukua hatua za kuishinikiza kiuchumi Ankara kupitia kuziongezea ushuru bidhaa za feleji za Uturuki zilizokuwa zinaingia Marekani. Hata baada ya mzozo huo kumalizika na serikali ya Uturuki kumuachilia huru kasisi huyo Mmarekani, lakini serikali ya Trump imesema kuwa haitoruhusu bidhaa hizo za Uturuki ziingie nchini humo kwa kiwango kile kile cha zamani cha ushuru. 
Amma kuhusiana na India ni kwamba uchumi wa nchi hiyo unakuwa kwa kasi kiasi kwamba India hivi sasa inahesabiwa kuwa ni dola la nne kwa kuwa na uchumi bora ulimwenguni. Suala hilo haliifurahishi Marekani ambayo daima inafikiria kuzikandamiza na kuzidumaza nchi nyingine. Hivyo Trump ameamua kuanzisha vita vya kiuchumi na India kama ilivyovianzisha dhidi ya China, Umoja wa Ulaya bali na hata Canada na Mexico. Siasa za Trump ni za kuzipandishia ushuru bidhaa za nchi hizo zinazoingia Marekani. Hivyo licha ya kwamba katika upande mmoja, Trump anaonesha hamu kubwa ya kustawisha uhusiano wake wa kiuchumi na India kutokana na soko lake kubwa, lakini wakati huo huo anaanzisha vita vya kibiashara na nchi hiyo ikiwa ni kuendeleza ubeberu ule ule wa kila siku wa Marekani dhidi ya mataifa mengine. Tab'a ni jambo lililo wazi kuwa India na Uturuki hazitonyamazia kimya siasa hizo mpya za kiuadui za Trump.
Ukweli wa mambo ni kwamba Donald Trump hatosheki na faida kubwa kupita kiasi anayoichukua kutoka kwa hata washirika wake wa jadi wa kibiashara na ndio maana kila siku anafikiria kupata faida mpya na kubwa zaidi bila ya kujali balaa linaloweza kuyafikia mataifa mengine. Kuzusha vita vya mara kwa mara vya kibiashara ni moja ya sifa kuu za serikali ya Donald Trump huko Marekani.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇