Askofu
Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo amewataka watu wasiogope kwenda au kuwapeleka wengine
kusoma katika Chuo cha Mtakatifu Joseph (SJUIT) kwa kuogopa
watalazimishwa kufuata imani ya chuo hicho kinachoongozwa kwa misingi
ya dini ya kikatoliki.
Askofu
Pengo amesema hayo jana Ijumaa Machi 8, katika mkutano wa kulitangaza
Baraza jipya la chuo lililotangazwa na Mkuu wa Chuo hicho uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
Alisema
licha ya chuo kuwa na malengo ya kikatoliki ambayo yana dini ndani yake
na kuna maeneo ambayo lazima yatabaki hivyo, haimaanishi kila
mwanafunzi anapaswa kubadili na kuwa mkatoliki.
“Mimi
nikija katika chuo hiki ntaingia kama Askofu na kama mkatoliki ambaye
ninaamini Yesu ni mwana wa Mungu, lakini hii haimaanishi kila anayekuja
kusoma hapa lazima afate misimamo yangu, kila mtu ana imani tofauti na
ana haki ya kuwa na imani tofauti.
“Jambo
la msingi ni kuwa na misimamo ya kidini ambayo inaongoza maisha ya
binadamu, na nitaendelea kusisitiza kuwa kila binadamu aliumbwa na Mungu
na maelekezo na maadili yote yanafundishwa kuhusu Mungu mmoja,
haijalishi ni dhehebu gani ila tunapaswa kujua Mungu huja kabla ya kila
kitu,” alisema Askofu Pengo.
Awali
akisoma majina ya baraza hilo jipya Mkuu wa Chuo hicho, Padri Arul Raj
aliwataka wajumbe wateule kufanya kazi zao kwa umakini wa hali ya juu
ili kukisaidia chuo kutoa elimu itakayozalisha wanafunzi bora ambao
wataisaidia nchi kukua katika nyanja mbalimbali hasa ya viwanda ili
kuendana na sera ya serikali ya ‘Tanzania ya Viwanda’.
“Lengo
la mwanzilishi wa chuo hiki ni kutoa wanafunzi wenye taaluma za Sayansi
na Teknolojia, hivyo sisi tumepewa dhamana ya kuhakikisha jambo hili
linatimia, hivyo basi inatupasa kuweka nguvu na akili zetu katika
kuzalisha wanafunzi watakao isaidia nchi ya Tanzania kukua hasa katika
sekta ya viwanda na uhandisi,”alisema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇