Na John Mapepele, Mpwapwa
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amemuagiza Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kuandaa haraka kanuni na mwongozo utakaosimamia kuanzia uvunaji wa mbegu, uuzaji, usambazaji na uhimilishaji na uhamilisha mifugo kabla ya mwezi Machi mwaka huu ili kuwadhibiti madalali wote wanaokwenda kuwaumiza wananchi kwa kutumia kivuli cha Serikali.
Akizungumza mara baada ya kutembelea Mradi wa uzalishaji kwa kutumia teknolojia ya viinitete na uhawilishaji (MOET) unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Kituo cha Mpwampwa mkoani Dodoma, Waziri Mpina alisema watanzania wajivunie mradi huo ambao ni wa kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Alisema kupatikana kwa teknolojia ya MOET kumeiwezesha Tanzania kuwa na njia tatu za kuboresha Koosafu ya mifugo ambapo ni njia ya asili ya kutumia madume bora, uhimilishaji (AI) na Uhamilishaji (MOET) ambapo itachochea mageuzi makubwa ya uboreshaji wa koosafu ya mifugo ambayo itaongeza uzalishaji wa maziwa, nyama, ngozi na mazao mengine ya mifugo.
Aidha aliagiza kuwa kila ifikapo mwezi Machi ya kila mwaka idara yake iwe imepeleka ajenda za kufanyiwa utafiti kwenye Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ili kupata matokeo ya tafiti ambazo watanzania wanaumiza vichwa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili na kuweka utaratibu wa kupokea tafiti kutoka nje ya nchi.
Pia amemwagiza Mkurugenzi huyo wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kukutana na wazalishaji wa mayai, vifaranga, ng’ombe, kuku, mbuzi, kondoo, punda, nguruwe, viwanda vya nyama, ngozi na maziwa ili kujua mahitaji yao kwa sasa ni yepi kwani wao ndio wataotengeneza ajenda za utafiti zenye uhitaji kwa sasa.
Amekosoa mfumo wa uendeshaji wa tafiti za mifugo nchini kwa kutokuwa na ajenda mahususi zinazohitajika kufanyiwa tafiti badala yake watafiti wengi wamekuwa wakiendesha tafiti za biashara kwa mataifa mengine ambazo hazina msaada kwa watanzania.
Amesema mfumo wa kuibua ajenda za utafiti haufahamiki huku kukiwa na ushirikishwaji dhaifu wa wadau hali inayosababisha tafiti nyingi kushindwa kutoa majawabu ya matatizo katika sekta ya mifugo nchini huku matokeo na mazao ya tafiti hizo yakiwafikia watu wachache kinyume na malengo ya Serikali.
Waziri Mpina alisema pamoja na kuwepo kwa njia zote hizo za uboreshaji Koosafu za mifugo bado kuna kasoro nyingi katika utaratibu unaotumika kuzalisha, kununua, kusambaza na kupandisha mifugo hali inayopelekea zoezi kuwa la kusuasua.
Alisema pamoja na mbegu hizo kuzalishwa na Serikali na kuuzwa mrija mmoja kwa sh 3,000 lakini kutokana na kutokuwepo mfumo madhubuti wa usimamizi na kuachiwa wafanyabiashara binafsi kwenda kuwauzia wafugaji kati ya sh 20,000 hadi sh 60,000 kwa mrija jambo linawakatisha tamaa wafugaji na kutofikiwa malengo ya Serikali.
Hivyo Waziri Mpina alisema juhudi zote zinazofanywa na Serikali za kuzalisha mbegu bora katika vituo vyake vya NAIC Arusha na Taliri Mpwapwa haitakuwa na maana kama kasoro zilizopo sasa hazitaondolewa.
Kwa upande wake Mkurungezi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Angello Mwilawa alimhakikishia Waziri Mpina kuwa atasimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo yake ili kuhakikisha wafugaji wananufaika na jitihada hizo zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika mkakati wake wa uboreshaji wa koosafu ya mifugo nchini.
Naye Mkurungezi Mkuu wa TARILI, Dk. Eligy Shirima alisema mradi huo wa MOET unafadhili na COSTECH kwa gharama ya sh milioni 400 kwa ajili ya kununua vifaa vitakavyowezesha kukamua mbegu za dume na kuziweka kwenye jike maalum lililoandaliwa.
Dk Shirima alisema jike hilo baada ya kuwekewa hormones husaidia mayai mengi kuiva kwa mara moja na kurutubishwa ambapo mbegu zilizorutubishwa hunyonywa na kuhifadhiwa na kisha kusambazwa kwa wafugaji kwa ajili ya uhamilishaji hatua ambayo itawezesha kupatikana mifugo bora.
Your Ad Spot
Feb 7, 2019
Home
Unlabelled
WAZIRI MPINA ATOA MAAGIZO MAZITO YA UHIMILISHAJI NA UHAMILISHAJI MIFUGO NCHINI
WAZIRI MPINA ATOA MAAGIZO MAZITO YA UHIMILISHAJI NA UHAMILISHAJI MIFUGO NCHINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇