Shirika la Ujasusi la Ufaransa DGSE lilikuwa na taarifa za kiitelijensia kuhusu njama ya mauaji ya rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, yaliyopelekea kuanza kwa mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.
Waraka wa kumbukumbu wa shirika hilo la kijasusi la Ufaransa uliochapishwa katika tovuti ya habari ya Medipart na idhaa ya Radio France kwa mara nyingine tena umethibitisha nafasi ya Ufaransa katika mauaji hayo ya kimbari ya Rwanda baada ya kupita miaka 24 tangu yatokee.
Kwa mujibu wa waraka huo, vyombo vya kijasusi vya Ufaransa vilikuwa na taarifa kwamba, Kanali Théoniste Bagosora, mpambe wa Waziri wa Ulinzi wa wakati huo na Laurent Serubuga, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda na ambao walikuwa na misimamo mikali, ndiyo waratibu na wachochezi wakuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda.
Oktoba mwaka jana, televisheni ya France 24 ilionesha mkanda wa video ulionukuliwa kutoka mtandao wa Media Party na kuripoti kuwa; mkanda huo wa video ambao ulichukuliwa na jeshi la Ufaransa, unaonesha jinsi askari wa Ufaransa walivyozembea na kujichelewesha kwenda katika eneo la Bisesero nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Serikali ya Rwanda imekuwa ikishikilia kwamba, Ufaransa ilihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo ya kimbari ambapo watu zaidi ya laki 8 waliuawa.
Itakumbukwa kuwa, mauaji ya kimbari ya Rwanda yalianza Aprili 6 mwaka 1994 baada ya kuuawa rais wa wakati huo wa nchi hiyo, Juvenile Habyarimana, kufuatia kutunguliwa ndege iliyokuwa imembeba karibu na uwanja wa ndege wa Kigali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇