Vyama vya upinzani nchini Sudan vinavyounga mkono maandamano dhidi ya serikali vimeitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa wito wa kujiuzulu Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo wakimtaja kuwa dikteta.
Taarifa ya pamoja ya vyama hivyo vya upinzani imeelezea wasiwasi mkubwa vilionao kuhusiana na mustakabali wa nchi hiyo hususan hali mbaya ya uchumi huku hali ikizidi kuwa mbaya tangu kuibuka maandamano nchi nzima dhidi ya serikali ya Khartoum.
Taarifa hiyo ya pamoja ya vyama vya upinzani ambayo ni ya kwanza imesisitiza kuwa, serikali ya Rais Omar al-Bashir inapaswa kuachia ngazi na kuruhisu kufanyika uchaguzi.
Jana maafisa usalama wa Sudan waliwatia mbaroni maprofesa na wahadhiri 14 wa vyuo vikuu vya nchi hiyo waliokuwa wakijiandaa kushiriki katika mgomo wa kukaa kitako kama sehemu ya wimbi la maandamano ya kupinga serikali ya Rais Omar al Bashir.
Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha sasa yamebadilika na kuwa ni wimbi la kumtaka Rais al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia uongozini.
Serikali ya Sudan imetangaza hali ya hatari katika baadhi ya mikoa ya nchi hiyo sambamba na kufunga shule na vyuo vikuu. Rais Omar al Bashir yuko madarakani nchini Sudan tangu mwaka 1993 ambapo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, muda wa mwisho wa kubakia kwake madarakani ni mwakani yaani 2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇