Kamati ya Kitaifa ya Palestina ya kuvunja mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza, imetangaza habari ya kufanyika maandamano ya 23 ya baharini karibu na kambi ya kijeshi ya Zakim, kaskazini mwa ukanda huo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Palestina, maandamano hayo ni sehemu ya shughuli zinazohusiana na maandamano ya kurejea, ambayo lengo lake ni kuvunja mzingiro wa kidhalimu dhidi ya eneo hilo. Maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' yalianza tarehe 30 Machi mwaka jana, kwa mnasaba wa 'Siku ya Ardhi' katika Ukanda wa Gaza na hadi sasa yangali yanaendelea. Kuendelea maandamano hayo kunasisitizia masuala tofauti katika kutetea haki za taifa la Palestina kutaka kuondolewa kikamilifu mzingiro wa kidhalimu dhidi ya eneo hilo. Katika fremu hiyo kufanyika maandamano ya baharini kwa ajili ya kuvunja mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza kunabainisha uwezo na azma ya dhati ya Wapalestina ya kupigania uhuru wao licha ya ukandamizaji wa kila aina na ukatili unaofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Wapalestina na kwa kutegemea uwezo tofauti wa kimuqawama, watakuwa wamefungua mrengo mpya kwa ajili ya kukabiliana na njama za Israel dhidi ya taifa lao. Hatua pana na zilizoratibiwa za wananchi katika kuvunja mzingiro wa eneo la Ukanda wa Gaza, zinazotekelezwa kwa sura tofauti, zikiwemo harakati za baharini, zimebainisha azma ya Wapalestina katika kukabiliana vilivyo na Wazayuni wanaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Ama lengo lingine la Wapalestina la kuanzisha maandamano ya baharini ya kuvunja mzingiro wa Gaza ni kuifikishia jamii ya kimataifa ujumbe huu kwamba, jamii hiyo imesalia tu kuwa mtazamaji wa hatua za ukiukaji wa haki na sheria za kimataifa unaofanywa na utawala huo khabithi wa Israel kama ambavyo katika uwanja huo, jamii hiyo haijachukua hatua yoyote ya maana katika kuwaunga mkono raia madhlumu wa Palestina. Inafaa kuashiria kuwa, Wapalestina wamechukua uamuzi huo ikiwa ni katika ubunifu wao binafsi. Tajriba ya mataifa mengi ambayo yaliwahi kupambana na dhulma na uvamizi, inaonyesha kwamba nao Wapalestina wanatakiwa waendeleze njia yao ya mapambano kwa ajili ya kurejea katika ardhi zao za asili zilizokaliwa kwa mabavu na utawala huo vamizi, sambamba na kufahamu kwamba kuzitegemea tawala tegemezi za Kiarabu au mazungumzo ya maridhiano na utawala wa Kizayuni, kamwe haviwezi kuwafanya waipate haki yao hiyo.
Katika mazingira hayo, Wapalestina wanasisitizia haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi ambapo hata maazimio ya kimataifa pia yanazitambua haki hizo ikiwemo ya kujiamulia mustakbali wao na kuundwa nchi huru ya Palestina. Kwa hakika, "Maandamano ya Baharini ya Kuvunja Mzingiro wa Ukanda wa Gaza", yametoa ilhamu na hamasa mpya kwa mapambano ya Wapalestina ya kuendesha muqawama wa kiraia sambamba na mapambano ya silaha katika kukabiliana na wavamizi wa Kizayuni. Aidha maandamano hayo ni yenye nafasi pana na yenye kutoa ujumbe wa wazi. Moja ya jumbe hizo ni kwamba taifa la Palestina lipo hai na kwamba njama yoyote ya kutaka kuanzisha mgogoro na kushadidisha mzingiro dhidi ya Wapalestina ili kuwatoa nje ya mkondo wa kusimama imara dhidi ya Israel kamwe haitofanikiwa. Ujumbe mwengine wa maandamano hayo ya baharini ni kwamba raia wa Palestina wameweza kwa kutumia ubunifu wao wenye lengo la kukabiliana na utawala wa Kizayuni, kuionyesha jamii ya kimataifa machungu na tabu wanazozipitia kutokana na jinai za utawala huo katili. Kwa hakika maandamano ya baharini kwa ajili ya kuvunja mzingiro wa Ukanda wa Gaza, ni changamoto mpya na njia iliyokuwa haijatarajiwa katika siasa zilizopewa istilahi eti za kiusalama za utawala haramu wa Kizayuni. Hatua hiyo ya Wapalestina imetoa ujumbe kwa Wazayuni kwamba changamoto za kiusalama bado zinaendelea kuusakama utawaa huo bandia unaoikalia kwa mabavu Quds licha ya kujizatiti na ngao ya kuzuia makombora na kuharibu njia za chini ya ardhi za Wapalestina.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇