Bunge la Marekani tayari limeshafungua uchunguzi dhidi ya pendekezo la utawala wa Trump, la kutaka kujenga vituo kadhaa vya kinyuklia nchini Saudi Arabia.
Mwakilishi Elijah Cummings, mwenyekiti wa Kamati ya Halmashauri ya Uangalizi na Mageuzi, ameitaka Ikulu ya Marekani kuwasilisha nyaraka ikiwa zile zinazohusu mkutano uliofanyika miezi miwili tu baada ya Trump kuingia madarakani kati ya mkwewe, Jared Kushner, na mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia , ambae muda mchache baada ya mkutano huo alitangazwa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Ripoti ya Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi imesema mshauri wa zamani wa usalama wa taifa Michael Flynn na wenzake wawili walipendekeza mpango huo kwa Tom Barrack, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya sherehe ya kuapishwa kwa rais, na muungano wa makampuni ya Marekani yakiongozwa na makamanda wa kijeshi waliostaafu na viongozi wa zamani wa Ikulu ya Marekani.
Juhudi za mpango huo, ripoti imesema zilianza kabla ya Trump kuingia madarakani na kuendelea hadi baada ya kuapishwa kwake Januari 2017, licha ya wafanyakazi wa Baraza la Usalama wa Taifa kuonya kwamba uhamisho wa teknolojia ya nyuklea ya Marekani kwenda Saudi Arabia unaweza kuangaliwa kama uvunjaji wa Sheria ya Nishati ya Atomiki.
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa na Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdelaziz, wakati wa ziara yake katika taifa hilo la kifalme.
Wabunge wamtaka Trump akae mbali na Salman
Mwanasheria wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la taifa John Eisenberg, aliamuru mpango huo usitishwe kwa sababu ya wasiwasi huenda Flynn akawa anavunja sheria kutokana na mgongano wa maslahi, kwa vile alikuwa mshauri wa muungano wa makampuni hayo yatakayofaidika na mpango huo, huku akiwa bado anatumika katika kampeni ya Trump na timu yake ya mpito. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti hiyo, ambayo imetumia ushahidi wa nyaraka tofauti na maelelezo ya watu waliofichua siri.
Ripoti hiyo imeongeza kwamba, uungwaji mkono kutoka katika serikali ya Trump hata hivyo unaendelea hado hivi karibuni, huku Trump akionekana wiki iliyopita kukutana na wawakilishi wa makampuni yanayotarajiwa kufaidika na mpango huo, katika ofisi yake ya Ikulu.
Wabunge wa Marekani, wakiwamo wa chama cha Trump cha Republican, wamekuwa wakiishinikiza Marekani kujiweka mbali na mwanamfalme Mohammed bin Salman kufuatia mauaji ya mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi. yanayodaiwa kuongozwa na taifa hilo la kifalme. Pia wanaitaka serikali ya Marekani, kusitisha kuviunga mkono vita vya Yemen, ambako mamilioni ya watu wako hatarini kutumbukia katika janga la njaa katika kile Umoja wa Mataifa inachokieleza kama mgogoro mbaya wa kibinadamu kushuhudiwa ulimwenguni.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afap,rtre
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇