Serikali ya Somalia imekanusha madai ya serikali ya Kenya kwamba imenyakua na kunadi maeneo ya mafuta yaliyopo katika mpaka unaozozaniwa kati ya taifa hilo na jirani yake huyo.
Katika taarifa yake rasmi, serikali ya Somalia imesema kuwa, 'haina mipango wala haikuwa na mipango ya kufanya hivyo'.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya kuwepo ripoti za kikao kilichofanyika katika mji mkuu Mogadishu cha maafisa wakuu serikalini akiwemo Rais mwenyewe Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo na Waziri Mkuu Hassan Ali Khayre.
"Somalia kwa sasa haina mpango wala haikuwa na mpango wa kunadi sehemu yoyote katika eneo linalozozaniwa baharini hadi pale Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) itakapobaini mipaka ya nchi husika," imeeleza taarifa hiyo rasmi.
somali
Aidha serikali ya Somalia imetoa ahadi kwa Kenya kuwa haitojihusisha na shughuli zozote katika maeneo yaliyopo kwenye mzozo baina ya nchi mbili hizo hadi pale mahakama ya ICJ itakapotoa uamuzi wa mwisho kuhusiana na mzozo huo.
Siku ya Jumamosi serikali ya Nairobi ilitangaza kuwa inamrudisha nyumbani balozi wake aliyepo Mogadishu Luteni Jenerali mstaafu Lucas Tumbo, ikidai kuwa uamuzi wa Somalia kupiga mnada eneo moja la mafuta mjini London wiki iliyopita ni sawa na uchokozi dhidi yake na mali yake asili.
Vilevile serikali ya Nairobi ilitangaza kumrejesha nyumbani balozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Nur katika kile ambacho serikali ya Kenya baadaye ilifafanuwa kwenye vyombo vya habari nchini humo kuwa ni kutoa fursa ya majadiliano ya kila upande katika suala hilo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇