LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 12, 2019

CHINA YAJIANDAA KUKABILIANA NA MELI ZA KIVITA ZA MAREKANI KWA MAKOMBORA YA DF-26

Jeshi la China limesimika makombora ya masafa ya kati aina ya DF-26 ya kushambulia meli katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya manuwari za kivita za Marekani kupita karibu na visiwa vya Paracel.
Makombora ya DF-26 yana uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia. Vilevile makombora hayo yanaeza kulenga maeneo yote ya bahari ya China Kusini. DF ni kifupi cha maneno mawili ya Dong-Feng yenye maana ya 'Upepo wa Mashariki.' Wamagharibi wanayaita makombora hayo kwa jina la "Muuaji wa Guam' (Guam Killer). Hii ni kwa kuwa serikali ya China inaweza kutumia makombora hayo ambayo yanaweza kwenda umbali wa kilometa 3000 hadi 4000, kushambulia kisiwa cha Guam chenye kambi za kijeshi za Marekani. Wachina wametangaza kuwa, makombora hayo yana uwezo wa kulenga shabaha nchi kavu na meli kubwa na za wastani za kivita na wakati huo huo kufanya mashambulizi ya silaha za nyuklia.
Kwa mujibu wa weledi wa mambo, hatua ya China ya kuweka makombora hayo ya DF-26 katika eneo hilo siku chache baada ya kupita manuari ya kivita ya Marekani ya USS Joseph E. Campbell karibu na visiwa vya Paracel katika bahari ya China Kusini, imetoa ujumbe kwa Marekani kwamba, hatua za kijeshi za Washington hususan katika Bahari ya China Kusini, zinaweza kuwa na madhara makubwa.
Meli ya kivita ya Marekani ikipita karibu na visiwa vya Paracel na kuibua chokochoko
Ukweli ni kwamba hatua hiyo ya China inaonyesha kuwa, serikali ya Beijing haipo tayari tena kufumbia macho hatua haribifu na za kichokozi za Marekani dhidi yake. Kuwekwa tayari makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia ya DF-26 kunaonyesha pia kwamba, China imeongeza utayarifu wake katika uga wa uwezo wa kijeshi.
Kuhusiana na suala hilo, John Mearsheimer mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Chuo Kikuu cha Chicago ameandika katika kitabu alichokipa jina la 'Janga la Madola Makubwa' kwamba: "China imejinoa kijeshi kwa kiasi ambacho hakuna nchi yoyote ya Asia inayoweza kutoa  changamoto hiyo na hizo ni juhudi za kutaka kudhibiti eneo hilo." Anaongeza kwa kusema kwamba: "Baada ya China kuongeza uwezo wake wa kijeshi, sawa na hatua zilizochukuliwa na Marekani katika karne ya 19 na kuzifukuza nchi za Ulaya kutoka bara la Amerika, sasa itaibainikia Washington kwamba, uingiliaji wake huko Asia haukubaliki tena."
Tunaweza kusema kwamba, kwa kuzingatia ongezeko la kila siku la uwezo wa kiuchumi wa China na kadhalika kuimarishwa nafasi ya nchi hiyo katika medani ya kimataifa, lengo la China kwa sasa ni kuimarisha uwezo wake zaidi ili ipate matumaini kwamba inaweza kukabiliana kijeshi na sera za kijeshi za Marekani.
Askari wa China wakiwa katika mazoezi ya kijeshi
Katika uwanja huo katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Beijing imepiga hatua kadhaa za kijeshi, ambapo uundaji wa meli ya kubeba ndege, makombora yenye kwenda kasi kubwa ya zaidi ya sauti, mifumo ya kisasa ya kujikinga na makombora, makombora yenye uwezo wa kuvuka bara na mikakati ya kutengeneza magari ya doria ya kizazi cha nne, ni sehemu ya maendeleo ya China katika uga wa kijeshi.
Pamoja na hayo, wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, licha ya kuzidisha uwezo wake wa kijeshi Beijing haina nia ya kuingia katika mapigano ya kijeshi au kuanzisha mashindano ya silaha. 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages