Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua chaneli mpya ya utalii itakayojulikana kama ‘Tanzania Safari Channel’ iliyoanzishwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mkurugenzi wa TBC, Dk Ayub Rioba amesema Rais Magufuli aliwapa wazo hilo mwaka jana.
Uzinduzi huo utafanyika Jumamosi Desemba 15, makao makuu ya TBC, Mikocheni, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa TBC, Dk Ayub Rioba akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 13 amesema chaneli hiyo itakuwa na vipindi vya vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Amesema uzinduzi rasmi wa chaneli hiyo utafanyika Jumamosi ukiongozwa na waziri mkuu, Kassim Majaliwa.
"Vipindi hivyo vitakuwa vinatoka kwa taasisi na wadau mbalimbali ikiwamo wa utalii, watozi (producers) wa ndani wa TBC, watozi binafsi wa ndani na nje na vile vinavyotengenezwa kwa pamoja na vyombo vingine vya utangazaji vya utalii (co-production)” amesema.
"Mchakato wa kuanzisha chaneli hii ulihusisha pia mikutano na wadau wa sekta binafsi ambao wanashughulika na masuala ya utalii,"
Amesema Rais John Magufuli alitoa wazo hilo alipotembelea makao makuu ya ofisi hizo mwaka jana ambapo uongozi wa TBC pia ilikuwa imeshaanza mchakato huo.
"Chaneli hii itakuwa inatangaza vivutio mbalimbali vya utalii nchini na kwa kuanza itaonekana kwenye king'amuzi cha Startimes,” amesema.
Amesema mipango iliyopo ni chaneli hiyo kuanza kuonekana kwenye satellite kwani lengo ni kuonekana katika nchi nyingi duniani ili kuvutia watalii wengi wa ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇