Ikiwa Zimesalia Siku 10 kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), vifaa vyote vya uchaguzi vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye ghala mjini Kinshasa vimetetea kwa moto hali inayozusha wasiwasi kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huo Desemba 23, 2018
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo, moto huo ulianza kuwaka saa 8 za usiku kwa saa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuteketeza vifaa zaidi ya 7000 yakiwemo magari ikiwa ni siku 10 tu kabla ya uchaguzi.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kwamba kabla ya moto huo kuwaka kulisikika mlipuko ambao unaaminika ndio chanzo cha moto.
Uchaguzi wa Disemba 23 nchini DRC umegubigwa na vurugu za kila namna ambapo jana watu wawili waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati Jeshi la Polisi likikabiliana na wafuasi wa mgombea wa upinzani Martin Fayulu katika Mji wa Kalemie.
Rais Joseph Kabila alisema kuwa ataondoka madarakani baada ya uchaguzi wa Disemba 23 wa kumtafuta mrithi wake, lakini akaeleza kuwa angebaki kwenye siasa na huenda akagombea tena huko mbeleni.
Mamlaka ya Rais Kabila aliyeiongoza DR Congo tangu mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent Kabila yalikoma mwaka 2016, lakini amekuwa akichelewesha uchaguzi, jambo ambalo limesababisha machafuko nchini humo.
Tume ya uchaguzi ilisema imekuwa vigumu kufanyika kwa uchaguzi kwa wakati nchini humo kutokana na changamoto za kuwaandikisha wapiga kura kunakochangiwa na uharibifu wa miundombinu na vita katika ukanda wa mashariki wa nchi hiyo.
Tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960, DR Congo haikuwahi kuwa na makabidhiano ya amani ya madaraka.
Kufuatia kuungua moto vifaa vya uchaguzi, watu wengi wanaamini kuwa tukio hilo linaweza kusababisha uchaguzi wa Disemba 23 kutofanyika tena kama ilivyopangwa, na Rais Kabila ataendelea kusalia madarakani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇