Kiwanda cha Samani cha Jeshi la Magereza jijini Arusha kimeteketea moto usiku wa kuamkia leo na kusababisha hasara kubwa kutokana na mashine mbalimbali pamoja na nyaraka mbalimbali kuungua.
Mara baada ya tukio hilo kutokea, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Kingu ambaye alikua safarini kuelekea wilayani Serengeti Mkoani Mara, kuhudhuria halfa ya uzinduzi wa Jeshi Usi la Tanapa, ilibidi ahairishe safari yake na kuelekea katika eneo la tukio hilo, Unga Limited jijini humo.
Katibu Mkuu Kingu alisema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme ambayo ilisababisha kiwanda hicho kuteketeza na kulisababishia Jeshi la Magereza kupata hasara kubwa pamoja na Wizara kwa ujumla.
Kingu alisema moto huo ulioanza saa 4 hadi saa 9 usiku wa kuamkia leo, uliteketeza jingo lililolokua na mashine mbalimbali za samani, mbao, ofisi ya Boharia na uhasibu na kusababisha nyaraka mbalimbali kuteketeza moto.
Aliongeza kuwa moto huo pia uliteketeza mabati ya jengo zima pamoja na kenchi za pande zote za jengo hilo ziliungua ambapo chanzo cha moto huo kinahisiwa kua ni hitilafu ya umeme katika swichi ya kuu ya jengo hilo.
“Mashine zilizoungua zinaweza kufanyiwa matengenezo makubwa na kurudi katika hali yake ya awali na kwa upande wa vipuli vilivyoungua vinahitaji kubadilishwa,” alisema Meja Jenerali Kingu.
Hata hivyo, Meja Jenerali Kingu alitoa wito kwa viongozi wa Jeshi la Magereza pamoja na taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya Wizara yake, kuchukua tahadhari za majanga yanayoweza kujitokeza kwa maana ya kuhakiki hali ya umeme ilivyo katika majengo yao pamoja na kuwa na vifafa vya kuzimia moto.
“Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha lina magari mawili ya zimamoto, na gari moja tu ambalo linafanya kazi mpaka sasa, hilo gari bovu tutalifanyia matengenezo ili kuwezesha uokozi pale linapotokea tukio la moto,” alisema Meja Jenerali Kingu.
Wakati Meja Jenerali Kingu akikagua maeneo mbalimbali yaliyoteketea kwa moto, aliambatana na Mkuu wa Magereza Mkoa huo, ACP Anderson, Mkuu wa Kiwanda hicho, SSP Victor Ngwale, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa huo, SSF Komba na Mwakilishi wa Jeshi la Polisi Mkoani humo, ACP Mnayama.
Kutokana na tukio la moto huo, pia Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike ambaye naye alikua ziarani mkoani Iringa, ameahirisha ziara yake na amewasili jijini Arusha kwa ajili ya kutafuta njia ya kukirudisha kiwanda hicho katika hali yake kutokana na hasara kubwa iliyotokea kutokana na moto huo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇