Mahakama moja nchini Marekani imeiagiza Ikulu ya White House kumrejeshea mwandishi wa habari wa televisheni ya CNN kibali ilichompokonya na kumzuia kuingia katika ikulu hiyo, baada ya kulumbana vikali na Rais Donald Trump.
Jaji Timothy Kelly wa Mahakama ya Federali ya Marekani jana Ijumaa aliaagiza White House kumruhusu ripota huyo wa CNN, Jim Acosta kuendelea kukusanya habari za White House hadi kesi kuhusu kadhia hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.
CNN na vyombo vingine vya habari ikiwemo televisheni ya Fox News ambayo Trump huishabikia mno viliunga mkono kesi hiyo ya Jim Acosta, vikisisitiza kuwa kupokonywa kibali cha kukusanya habari za White House ni ukiukaji wa haki zake za msingi na kubinywa uhuru wa vyombo vya habari.
Hivi karibuni, Trump na mwandishi habari huyo wa CNN walitupiana cheche za maneno na kisha usimamizi wa White House ukampokonya ripota huyo kibali cha kuingia ikuluni hapo.
Ofisa mwanamke wa White House alionekana akijaribu kumpokonya kipaza sauti mwandishi huyo baada ya kurushiana maneno makali na Trump. Trump alikataa kujibu maswali ya ripota huyo, akimtuhumu kuwa ni mtu jeuri na kwamba chombo chake cha habari (CNN) kinaeneza habari feki na za kipropaganda dhidi ya utawala wake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇