Watu wasiopungua 55 wameuawa katika mapigano ya kidini jimboni Kaduna, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Ahmad Abdur-Rahman, Kamishna wa Polisi katika eneo hilo amesema leo Jumapili kuwa, watu hao wameuawa katika mapigano yaliyoshuhudiwa ndani ya siku chache zilizopita katika mji wa Kasuwan Magani, kusini mwa jimbo la Kaduna.
Ameongeza kuwa, watu 22 wametiwa mbaroni wakihusishwa na ghasia hizo na kwamba agizo la kutotoka nje lililotolewa na vyombo vya usalama siku ya Alkhamisi limesaidia kupunguza taharuki na mchafukoge katika eneo hilo.
Garba Shehu, Msemaji wa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema mwenendo huo wa ukatili jimboni Kaduna unatia wasiwasi huku akisisitiza kuwa, tofauti zinazopelekea kushuhudiwa mapigano hayo ya kidini na kikabila zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia za amani.
Mapigano ya kidini na kikabila yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria.
Inaarifiwa kuwa, zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita kutokana na mapigano yanayosababishwa na tofauti za kidini nchini humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇