LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 21, 2018

UTURUKI YATISHIA KUFICHUA KWA VYOMBO VYA HABARI UCHUNGUZI KUHUSU FAILI LA KASHOGGI

Mevlut Cavusoglu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ametishia kuwa matokeo ya uchunguzi kuhusu faili la kutoweka mwandishi habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi yatakabidhiwa kwa uwazi kwa vyombo vya habari.
Kuhusiana na uchunguzi unaofanywa kuhusu kutoweka mwandishi habari wa Saudia Jamal Khashoggi; Mevlut Cavusoglu ametangaza kuwa serikali ya Ankara ina taarifa na nyaraka muhimu kuhusu hatima ya mwandishi huyo na kwamba itakabidhi matokeo hayo kwa vyombo vya habari  na kwa fikra za waliowengi duniani baada ya uchunguzi kukamilika. 
Mavlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki 
Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki yanapaswa kutajwa kama sehemu nyingine ya mashinikizo ya Uturuki kwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia. Kabla ya hapo, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki pia alitoa tishio sawa na  hili la waziri wake dhidi ya Saudi Arabia. Inaonekana kuwa viongozi wa Uturuki wanataka kufikia mapatano nyuma ya pazia na Saudia ili kunufaika zaidi na kadhia hii. 
Kuhusiana na suala hili, Marekani ikiwa muungaji mkono mkuu na muhimu wa utawala wa kifalme wa Saudia pia inakabiliwa na hali ngumu hivi sasa. Kwa mfano maseneta kadhaa wa Marekani wametaka kutolewe radiamali kali, serikali ya Marekani ifuatilie kadhia hii ya kuuliwa mwandishi habari ambaye alikuwa akiikosoa Saudia na Riyadh itoe jibu kuhusiana na mauaji haya. Bob Corker Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Nje katika Seneti ya Marekani amekosoa msimamo wa White House kuhusu kuuliwa mwandishi huyo wa habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia na kusema: Kubadilika mara kwa mara misimamo ya viongozi wa Saudi Arabia kuhusu kuuliwa Jamal Khashoggi ni jambo lisilokubalika. 
Bob Corker, Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Nje katika Seneti ya Marekani 
Tim Kaine seneta wa chama cha Democrat cha nchini Marekani pia amesema: Maelezo yanayotolewa kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi ni udhalilishaji na unyama huu unapasa kukomeshwa. Katika mazingira haya hakuna shaka kuwa Uturuki huku ikifanya juhudi za kufikia mapatano nyuma ya pazia na utawala wa kifalme wa Saudia inataka kufikia mapatano pia na Marekani kwa maslahi yake. Uturuki imeshindwa kufikia matakwa yake kutoka kwa Marekani baada ya kumuachia huru padri jasusi wa Kimarekani. Kwa msingi huo viongozi wa serikali ya Ankara wanafanya juhudi za kuziweka chini ya mashinikizo Marekani na Saudi Arabia kwa wakati mmoja kutokana na  mgogoro huu mpya unaowakabili. 
Ukweli ni kuwa uhusiano wa Uturuki na utawala wa kifalme wa Saudia na Marekani umevurugika na umekuwa wa mivutano  katika kipindi cha miaka ya karibuni. Ndio maana inaonekana kuwa viongozi wa Ankara wanafanya kila linalowezekana kuhuisha uhusiano wao na Washington pamoja na Riyadh. Tishio lililotolewa na viongozi wa Ankara kwamba watafichua kwa vyombo vya habari kashfa ya kutoweka na kisha kuuawa kwa mwandishi Jamal Khashoggi ni katika jitihada za kuziweka chini ya mashinikizo Marekani na Saudia ili waweze kufikia matakwa yao. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages