Rais John Magufuli leo Oktoba 4, 2018 amepokea hati za utambulisho wa mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, mabalozi hao ni kutoka Palestina, Kuwait, Norway, Ubelgiji na Sweden.
Rais Magufuli amepokea hati hizo Ikulu jijini Dar es Salaam.Miongoni mwa watu waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga na viongozi wengine.
Mabalozi hao walipowasili Ikulu kila mmoja kwa wakati wake kwa msafara maalum wa askari polisi wenye pikipiki, walipigiwa wimbo wa taifa kabla ya kuendelea na hatua ya kukabidhi hati.
Mara baada ya kila mmoja kuwasilisha hati zao, wamefanya mazungumzo na Rais Magufuli kwa muda mfupi kisha kutoka na kupigiwa wimbo wa Taifa huku gari aliloingia nalo, linapandishwa bendera ya nchi yake wakati anaondoka.
Balozi wa Norway kabla ya kuja nchini alifanya kazi nchini Afghanistan kwa miaka mitano huku wa Kuwait alifanya kazi Romania na Marekani
Katika utambulisho huo, balozi wa Palestina alimsalimia Rais Magufuli kwa lugha ya Kiswahili akichanganya na Kiarabu.
“...Asalamu aleykum, nimefurahi kukutana na Rais wa Tanzania...” alisikika akisema
Mara baada ya mabalozi hao kumaliza kupokea hati, Balozi Mahiga amesema Rais Magufuli amemsisitiza Balozi wa Norway kuikumbusha nchi yake kumaliza mapema mazungumzo kuhusu kampuni ya State oil na Sheli.
Amesema mazungumzo hayo yanayoendelea kwa kusuasua, lengo lake ni kampuni hizo mbili kushirikiana kujenga kiwanda cha kuchakata gesi ili iuzwe nje ya nchi.
Balozi Mahiga amesema eneo la kujenga kiwanda limeshapatikana na gesi pia ipo, hivyo mazungumzo hayo yakikamilika kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.
Kuhusu ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji (Stiegler's Gorge), Rais Magufuli amemwambia balozi wa Sweden mbuga ya Selous haina manufaa kwa Tanzania bali kwa ulimwengu mzima.
“Rais amemueleza ni asilimia 1.3 ya eneo la mbuga ya Selous ndiyo limetumika kwenye mradi huo, ambao ni muhimu kwa sababu ukikamilika utawahakikishia Watanzania nishati ya umeme, tofauti na hapo wataendelea kukata miti na hata hiyo mbuga haitakuwapo tena, ”amesema Balozi Mahiga.
Amesema Rais Magufuli amemweleza Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo imetenga asilimia 32.5 ya ardhi yake kwa ajili ya hifadhi ya misitu na wanyama.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇