Na Ismail Ngayonga, MAELEZO
KATIKA kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa wananchi, Serikali imeweka mazingira rafiki ya kisera na ya kisheria ya kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, kudumisha hali ya amani, utulivu na utangamano wa kitaifa.
Serikali kupitia Mahakama ya Tanzania inatekeleza Mpango Mkakati wa Maboresho ya Mahakama miaka unaolenga kuboresha huduma zinazotolewa kwa wadau na wateja ili kuifanya Mahakama kuwa ya kisasa na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
Mpango huo unaotekelezwa katika kipindi cha miaka 5 (2015-2020) pamoja na mambo mengine umekusudia pia kuifanya Mahakama kuendesha shughuli zake kwa muundo wa mahakama za kimataifa ikiwa ni mwanzo wa kufikia malengo matatu yenye matokeo makubwa 17 katika uendeshwaji wa mahakama nchini.
Maboresho hayo yameeenda sambamba na kuongeza Mahakama Kuu 7, uanzishwaji wa mahakama za wilaya 108 katika wilaya 28 na Mahakama za mwanzo ili kuwawezesha watanzania millioni 21 ambao wanatokea katika maeneo ambayo hayana mahakama hizo kupata huduma.
Wadau na wananchi mbalimbali nchini wamekuwa na malalamiko mbalimbali kuhusu utaratibu mzima wa uendeshaji wa kesi Mahakamani, na kuelekeza tuhuma kwa Mahakama kuwa ndiyo inayosababisha kesi kuchukua muda mrefu mpaka kumalizika ikiwemo na dhana ya upokeaji wa rushwa kwa baadhi ya watumishi wa Mahakama wasio waaminifu.
Aidha kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka kuwa Mahakama inachelewesha kesi bila sababu za msingi, ambapo malalamiko haya yamekuwa yakitolewa kwa njia mbalimbali kupitia magazeti, runinga, mitandao ya kijamii na Makongamano.
Aidha Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Serikali imeendelea kufanya tathmini ya hali ya utekelezaji wa sheria nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinakwenda sambamba na mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu aktika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Katiba na Sheria, Palamagamba Kabudi anasema kwa muda mrefu suala la kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani limekuwa ni moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata haki kwa wakati.
Prof. Kabudi anasema hadi kufikia mwezi machi 2018, Mahakama imeamua jumla ya mashauri 141,107 katika ngazi zote za Mahakama sawa na asilimia 98 ya mashauri yaliyosajiliwa katika kipindi hicho, na asilimia 67 ya mashauri yote yaliyokuwepo mahakamani kwa kipindi hicho.
“Katika kupunguza mlundikano wa mashauri, Serikali kupitia Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika Mahakama za Mwanzo, Wilaya na za Hakimu Mkazi, mafanikio haya ni matunda ya utaratibu waliojiwekea Waheshimiwa Majaji na Mahakimu wa kuweka ukomo wa chini wa idadi ya mashauri anayotakiwa kuamua Jaji au Hakimu” anasema Prof. Kabudi.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi anasema kupitia Mpango wa Maboresho, Mahakama ya Tanzania imekusudia kuweka mifumo imara na ujenzi wa miundombinu ya utoaji huduma ikiwemo ujenzi wa Mahakama za Wilaya za Bagamoyo, Ilala, Kigamboni na Mkuranga na kuanza ujenzi wa Mahakama Kuu katika Mikoa ya Kigoma na Mara.
Anaongeza katika kuhakikisha na kuongeza fursa ya upatikanaji wa haki kwa wakati Mahakama ya Tanzania imeboresha na inaendelea kuboresha miundombinu ya majengo ya Mahakama katika ngazi zote kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu mijini na vijijini.
“Mahakama inaendelea na ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Geita, Njombe, katavi, Lindi na Simiyu, Mahakama za Wilaya 16 na kukamilisha ujenzi wa Mahakama za Mwanzo nane, pamoja na Mpango wa kuwa na Mahakama Kuu kila Mkoa, Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa yote nchini” anasema Prof. Kabudi.
Ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati; Majaji na Mahakimu vyema waweke utaratibu na mpango maalum ikiwa ni pamoja na kuwa na idadi maalum ya kesi ambazo wanatakiwa kuzisikiliza na kuzimaliza kwa mwaka pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu taratibu na hatua za kesi inapotia Mahakamani ikiwa ni pamoja na kufanyiwa kazi kwa pamoja na wadau wake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇