Na WAMJW – KAGERA, NGARA
Serikali kupitia Wizara ya Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kuweka mikakati thabiti katika maeneo yote hatarishi ikiwemo mipakan na njia za panya ili kudhibiti ugonjwa wa Ebola kuingia nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu jana wakati alipofanya ziara katika Mpaka wa Rusumo kati ya nchi ya Tanzania na Rwanda ili kuangalia ni jinsi gani Mkoa wa Kagera umejipanga katika kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kuingia nchini.
Waziri Ummy amesema kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umetokea eneo la Kivu katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo unaiweka Tanzania katika hatari zaidi ya kuweza kupata wagonjwa wa Ebola kutokana na muingiliano wa wananchi baina ya nchi hizo.
“Mlipuko huo wa Ugonjwa wa Ebola ambao umetokea katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo sasa hivi inatuweka Tanzania katika hatari kubwa zaidi kupata wagonjwa kutokana na mlipuko huo kutokea eneo la Kivu Kaskazini ambalo ni karibu na Tanzania na muingiliano wa wananchi baina ya nchi hizi mbili ni mkubwa ” Alisema Waziri Ummy Mwalimu.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa wahudumu wa Sekta ya Áfya ili kufahamu jinsi ya kuwahudumia wanaohisiwa kuwa na Virusi vya ugonjwa wa Ebola sambamba na hilo Serikali imeleta vifaa kinga watakavyovaa wakati wakitoa huduma kwa mgonjwa au mhisiwa wa ugonjwa wa Ebola.
“Kama Serikali, kubwa ambalo tumelifanya ni kuhakikisha tunatoa mafunzo kwa watoa hudumu wa sekta ya Áfya nchini.kwa mujibu wa taarifa ya WHO nchini Kongo watoa huduma wa Áfya 9 wamepata ugonjwa wa Ebola huku mmoja amefariki” Alisema Waziri Ummy.
Pia Waziri Ummy alimwagiza Mkuu wa mkoa wa Kagera kuhakikisha wanatenga Zahanati moja katika maeneo ya mipaka ambayo itakuwa inapokea wahisiwa au wagonjwa wa Ebola, vivyo hivyo kwa ngazi ya Wilaya kutenga hospitali kwa ajili ya wahisiwa pindi utapoingia nchini.
Hata hivyo h Waziri Ummy amewataka wananchi wanaokaa katika vijiji vya mipakani ambavyo vinapokea watu kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Burundi wamuonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola wamwelekeze kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya vilivyo jirani.
” Wananchi ambao wanakaa mipakani hasa katika vijiji ambavyo vinapokea watu kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Burundi mnaowajibu wa kuhakikisha mnafuata taratibu za uhamiaji, lakini pale ambapo mtu ameingia na ana dalili za ugonjwa wa Ebola muelekezeni aende kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya” alisema Waziri Ummy
Kwa upande mwingine Waziri Ummy alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Áfya imeajiri Watumishi wapya wa Sekta ya Áfya 33 ambao wamesambazwa kwenye maeneo ya mipakani ili kusaidia kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini.
“Zuli ambalo tumelifanya, tumeajiri watumishi wapya wa Áfya 33 kwa ajili ya kuwasambaza katika maeneo haya ya mipakani ili kudhibiti ugonjwa huu wa Ebola usiingie nchini kwetu” alisema Waziri Ummy.
Mbali na hayo Waziri Ummy amekiagiza kitengo cha Elimu ya Áfya kwa umma kutoka Wizara ya Áfya kutoa Elimu juu ya ugonjwa wa Ebola kwenye Serikali za vijijini kupitia Redio, vipeperushi, video jambo litalosaidia kuweka msukumo kwa wananchi ili kujua athari za ugonjwa huo kwa maendeleo ya Taifa.
Mwisho Waziri Ummy aliendelea kuwatoa hofu wananchi wa Tanzania kuwa ugonjwa wa Ebola bado haujaingia nchini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇