Dar es Salaam
"Nimekuja na mikakati na malengo yangu ya kusimamia uongozi ili kuleta mageuzi chanya katika vyombo hivi vya habari vya chama, nipeni muda walau miezi mitatu hivi niwasome na ninyi mnisome halafu tuelewane namna ya kwenda pamoja katika kuleta mageuzi haya.
Kwa sasa sitasikiliza maoni au hoja zetu kwanza, nahofia nikifanya hivyo nitatoka kwenye 'reli' ya mikakati niliyopanga, fanyeni kazi zenu kwa bidii na maarifa katika namna ile ile mliyozoea, wakati mimi nikiwa katika maandalizi ya kufanya mageuzi nilivyopanga kufanya", alisema Ernest Sungura wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika Chumba cha Habari cha Uhuru Publicatiosn Ltd, Wachapishaji wa Magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, wakati akitoa maoni katika sehemu ya mengineyo kwenye kikao cha kawaida cha kikazi cha mapitio ya magazeti, jana.
Anasema, anatambua kuwa baada ya kutangazwa rasmi kuwa Msimamizi Mkuu wa Vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wengi ndani na nje ya Chama na hasa wana tasnia ya habari wanayo matumaini makubwa ya kushuhudia mageuzi chanya kwenye vyombo hivyo vya habari vya Chama.
"kwa sababu hivyo nitahakikisha natumia weledi wangu wote kuona kwamba kwa kushirkiana nanyi na wadau wengine matumaini waliyonayo hawa watu yanatamalakini, ni lazima nihakikishe nalinda heshima niliyonayo katika tasnia ya habari na ile niliyopewa na Chama kushika jukumu hili", alisema Sungura.
Naam, ikiwa ni katika hatua za Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk John Magufuli kuleta mageuzi chanya katka serikali na ndani ya Chama, hatimaye Kamati Kuu ya CCM katika kikao chake cha hivi karibuni ilimteua na kuridhika kuwa Kada mahiri wa CCM Ernest Sungura atatosha kulibeta jukumu la kuvivusha vyombo vya habari vya chama kutoka katika dhiki ya kudidimia na kukabiliwa na hofu ya kufa kwa kipindi kirefu sasa.
Ni jambo la faraja kwamba kama alivyoeleza mwenyewe Sungura ni kwamba katika kuwa nje ya kufanya moja kwa moja kazi za uandishi wa habari akiwa Mkurugenzi wa Mfuko wa vyombo vya Habari na kwingineko ameweza kujua madhaifu na shida mbalimbali vya vyombo vvya habari hapani vikiwemo vya Chama.
Pamoja na imani hiyo inayojengwa na wadau kutokana na kuamini kuwa Sungura anazitambua shida zinazovikabili vyombo vya habari vya Tanzania na hasa vya CCM bado ukweli unabakia kwamba dhamira yake ndiyo pekee itakayokuwa nyenzo kuu ya kufanikisha ustawi wa vyombo vya Chama katika jukumu alilopewa, hii ni kwa sababu wapo wengi waliwahi kupewa jukumu hili, lakini hawakuweza kuonyesha matokeo chanya.
Kabla ya uteuzi, Sungura alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa vyombo vya habari Tanzania (TMF) lakini aliondolewa katika taasisi hiyo na Bodi yake (TMF) muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi.
Sungura ndiye mwasisi wa Tanzania Media Foundation (TMF), taasisi iliyoleta mageuzi makubwa katika tasnia ya habari nchini na kuifanya nchi jirani ya Kenya kuja kujifunza nchini kabla ya kuanzisha taasisi kama hiyo nchini mwao.
Basi, ikiwa aliweza kusimamia dhamira yake na kuifanya TMF kufanya mageuzi makubwa katika tasnia ya habari nchini kwa kiwango cha kuifanya Kenya kuja kujifunza kabla ya kuanzisha taasisi kama hiyo nchini mwao bila shaka halitakuwa neno kubwa kwa Sungura kuleta mageuzi chanya kwenye vyombo vya habari vya CCM ambavyo ni pamoja na televisheni, redio, magazeti na mitandao.
Imani hii kwa Sungura inatokana na kwamba pamoja na mafanikio mengine, Sungura amekuwa na rekodi nzuri na ya kipekee katika kuleta mageuzi ya kimkakati kwa taasisi za habari nchini.
Baadhi ya mafanikio makubwa yameonekana katika kuzipatia taasisi hizo uongozi na menejimenti madhubuti, hivyo kuleta maboresho katika maudhui, miundo na mifumo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha vyanzo vya mapato na kusaidia vyombo vya habari kujiendesha kama taasisi kamili zinazopata faida.
Sungura ana uzoefu wa zaidi ya miaka 24 (1994-2018) katika tasnia ya habari nchini, hasa katika kuwajengea uwezo wanahabari vijana huku akibuni program mbalimbali za kuijenga na kuiimarisha tasnia ya habari.
Amekuwa anajulikana kwa wengi kama kiongozi mahiri mwenye kujali matokeo, kocha, menta (mentor), mshauri wa kitaalam na mwalimu na pengine ilichangia kumfanya ang'are zaidi hadi kumfanya Disemba 2017, kuchanguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na baadaye Mwezi Mei mwaka huu, kuwa miongoni mwa wajumbe tisa ambao Mwenyekiti wa CCM Dk John Magufuli ilimpendeza na kuwapendekeza kugombea nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Kwa namna inavyoweza kuonekana ni kwamba kwa kulipendekeza jina na Komred Sungura katika majina hayo tisa kugombea ujumbe wa Kamati kuu ya CCM, Mwenyekiti wa CCM Rais Dk Magufuli alikuwa katika kumsaka ili kusaidia kutimiza dhamira yake ya kuleta mageuzi katika vyombo vya habari vya chama ili kuvifanya kuwa mshindani mzuri katika sekta ya habari ikiwa ni pamoja na kuwa mhimili katika kusaidia mabadiliko ya kiuchumi nchini, ambapo Rais alitoa ahadi ya hamira hiyo wakati akichukua uongozi wa Chama.
Rais Dk Magufuli bila shaka aliahidi na kuendelea kutekelza dhamira hiyo kwa kuwa anatambua kuwa Sekta ya habari na mawasiliano ni muhimu sana katika siasa za dunia, ikiwemo Tanzania, hasa katika kutoa ushawishi na uungwaji mkono wa mikakati na sera za Chama cha kisiasa kwa umma.
Hivyo kwa kutambua hivyo ilimpasa kuhakikisha Msimamizi Mkuu wa Vyombo vya habari vya chama lazima awe mtu wa aina ya Sungura ambaye kupitia TMF aliweza kuchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio chanya yanayoonekana katika tasnia ya habari hapa nchini katika muongo mmoja uliopita.
Sungura ni miongoni mwa wanahabari makini na wenye rekodi ya ufuatiliaji ambao wamepitia mafunzi katika fani zaidi ya uandishi wa habari, ana uwezo mkubwa, amebobea katika fani ya habari, usimamizi wa biashara, mafunzo ya wanahabari, ikiwa ni pamoja na uandaaji wa mikakati na pia ni mtu asiyeshindwa jambo analokabidhiwa, hakika CCM imefanya uchaguzi sahihi.
Kutokana na uchapakazi wake, Komredi Sungura amewahi kufanya kazi na taasisi za kimataifa kama vile Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika kuboresha matangazo ya vyombo vya habari vya umma (Public Broadcasting Services) kama vile TBC na ZBC, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa.
Sungura ni msomi ambaye ana Digrii ya Uzamili katika usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam, Digrii ya Kwanza katika Usimamizi wa Biashara kutoka katika Chuo hicho hicho na Diploma ya Uandishi wa Habari kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania, TSJ (sasa SJMC).
Your Ad Spot
Aug 8, 2018
Home
Unlabelled
ERNEST SUNGURA KATIKA TASWIRA YA RAIS DK. MAGUFULI KUBORESHA VYOMBO VYA HABARI VYA CHAMA
ERNEST SUNGURA KATIKA TASWIRA YA RAIS DK. MAGUFULI KUBORESHA VYOMBO VYA HABARI VYA CHAMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇