LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 30, 2018

WAZIRI MKUU:GEREZA LA KWITANGA KUWA KITUO KIKUU CHA MICHIKICHI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeliteua Gereza la Kwitanga lililopo wilayani Kigoma kuwa kituo kikuu cha uzalishaji wa zao la michikichi nchini.

Hivyo ameuagiza uongozi wa gereza hilo waongeze nguvu katika uzalishaji wa michikichi kwa kupanua mashamba na kuongeza askari wenye ujuzi wa kilimo cha michikichi na kupanda miche mipya ya michikichi na kukata ya zamani.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 29, 2018) wakati alipotembelea gereza hilo akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi yenye lengo la kufufua zao la michikichi mkoani Kigoma.

Amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kufufua kilimo cha zao la michikichi mkoani Kigoma, hivyo kila mwananchi lazima awe na shamba la michikichi.

Katia hatua nyingine, Waziri Mkuu ameuagiza Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma Bw. Sabas Matolo kuhakikisha Gereza la Kwitanga linawezeshwa kwa kuwa na zana bora na za kisasa za kilimo yakiwemo matrekta na vifaa vya kuvunia ili waweze kuongeza uzalishaji wa mafuta.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Bw. Matolo awahamishe askari  ambao ni wataalamu wa kilimo wenye ujuzi wa zao la michikichi kutoka kwenye Magereza mengine mkoani Kigoma  na kuwahamishia katika gereza la Kwitanga ili kuimarisha uzalishaji.

Awali, Mkuu wa gereza hilo Bw. Majuto Masila alisema ili kilimo cha michikichi na uzalishaji wa mafuta uweze kuwa na tija, wanahitaji wafungwa wasiopungua 300 wawepo kila siku gerezani hapo ili kumudu shughuli za shamba hilo. Kwa sasa kuna wafungwa 112.

"Uzalishaji wa mafuta kwa miaka mitatu mfululizo gerezani Kwitanga ni kama ifuatavyo mwaka 2015/2016 tulizalisha lita 16,094, mwaka 2016/2017 lita 12,674, na mwaka 2017/2018 tulizalisha lita 16,000,"  alisema.

Alisema mafuta yanayozalishwa gerezani hapo yanatumika katika kulisha wafungwa wa gereza hilo la Kwitanga, Bangwe, Kasulu, na Kibondo. Ziada ya mafuta hutumika kulisha wafungwa magereza ya mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga, Singida, Dodoma, Morogoro na Tabora.

Baada ya kutoka katika Gereza la Kwitanga, Waziri Mkuu alitembea shamba darasa na eneo la kuzalisha miche ya michikichi la Seed Change katika eneo la Mungonya na kuziagiza halmashauri zote zinazolima michikichi mkoani Kigoma kwenda kununua mbegu kwenye shamba hilo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages