LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 30, 2018

MWANDISHII WA HABARI AFARIKI DUNIA, NI SHADRACK SAGATI

SIKUJUA KUWA ULIKUWA UNANIAGA SHADRACK SAGATI, LALA SALAMA


Na Derek Murusuri
AKIWA  anafundisha katika mojawapo ya shule za msingi za jiji la Dar es Salaam, zaidi ya miaka 22 iliyopita, niliuona uwezo mkubwa wa uchambuzi ndani ya SHADRACK SAGATI, afisa wa habari katika Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji ambaye amefariki ghafla usiku wa Jumatatu (30-7-2018).

“Unastahili kuwa mwandishi wa habari. Kuna fursa nyingi za kujiendeleza katika uandishi wa habari. Jiandae, nitakusaidia kama utakuwa tayari ili uje usome katika chuo cha uandishi wa habari ninachofundisha,” nilimwambia Sagati.

Tulikuwa tumemaliza ibada ya Sabato, katika Kanisa la Waandventista wa Sabato la Magomeni Mwembechai ambapo yeye alikuwa akihudumu kama mwanakwaya katika kwaya ya Kanisa hilo.

Mwalimu Sagati alinisikiliza kwa makini na maneno yangu yalimwingia na kuuchoma moyo wake. Alitaka kujua ni namna gani ataweza kumudu kulipa ada na pia kazi yake ya ualimu wa shule ya msingi.

“All things are possible,” nilimwambia. Alishawishika palepale. Ndani ya muda mfupi alikuwa mwanafunzi wa cheti wa chuo cha uandishi wa habari cha Serikali (TSJ) na kuanza safari yake ya mafanikio makubwa katika fani ya uandishi wa habari hapa Tanzania.

Akiwa kijana mwenye akili nyingi, fikra pevu, mwenye bidii na hekima, Shadrack Sagati aliitumikia vema sana fani ya uandishi hadi kuwa mwandishi wa kutegemewa katika habari zinazohusu matukio makubwa ya kitaifa katika gazeti la Serikali la Habari Leo.

Wakati nikiwa nawakilisha taasisi Uingereza ya elimu ya biashara hapa nchini, The Association of Business Executives (ABE), Sagati alinipa ushirikiano wa hali ya juu sana. Nilizidi kugundua kuwa alikuwa mtiifu na pia hakusita kutoa ushauri wa kuboresha pale ilipobidi.

Siku moja nilimpigia simu kumpa habari. Wakati sakata la “the northen corridor”, pale “coalition of the willing”, wakiwa wamezimia kwenda bila Tanzania, nikatoa maoni yangu kuhusu ushirikiano mbadala wa Tanzania, Burundi, DRC na Comoro.

Aliandika habari katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la Habari Leo. Bungeni Marehemu Kepteni Komba na wabunge wenzake wakaibeba hoja hiyo na kulifanyia kazi.

Rais wa wakati huo, Mhe Dk Jakaya Kikwete aliona vema kwenda Bungeni na kwa hekima yake akalihitimisha suala hilo. Sagati alijaaliwa akili na wepesi wa kuchakata habari. Alijua habari nzuri iko wapi. Hakika aliendeleza kipaji cha ualimu katika fani ya habari.

Sagati hakuwa mwandishi wa kawaida. Alivuka viwango hivyo. Alikuwa mtu mwenye malengo makubwa. Kwanza alianza kwa kujiendeleza kielimu. Mbali na kurudi tena chuoni ili kuwa mahiri katika uandishi wa habari, Sagati alikwenda mbali zaidi na kupata Shahadi ya usimamizi wa biashara (Bachelor of Business Administration) katika chuo cha elimu ya biashara (CBE).  Alianza masoma ya Shahada ya Uzamili.

Elimu ya biashara ilimsaidia kufanya tathmini nzuri na za kuvutia ambazo pia zilitumiwa na viongozi mbalimbali wa biashara na siasa. Wengi walimwita kwa ushauri na kuripoti habari zao kwa vile waliamini katika weledi wake na tunu zilizomuongoza katika maamuzi yake.

Alijijengea mazingira ya kuaminiwa. TRUST huja baada ya mwandishi kujipambanua katika uandishi wake na kuonesha umahiri. Weledi wa Sagati ulikuwa kielelezo cha uandishi bora nchini.

Takriban wiki tatu zilizopita, nilimpigia simu Shadrack kuhusu jambo moja. Aliniambia kuwa alikuwa safarini akitokea Dodoma kurudi Dar. Aliniambia habari njema na alikuwa mwenye furaha sana. Mwanafalsafa Abraham Maslow, anasema, “self actualization,” kiwango cha juu unachofika katika wakati maalum.

“Nimepewa mapumziko ya wiki moja kupisha mchakato wa kunihamishia Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji,” alinieleza kwa furaha.

Lakini, alinishangaza sana kuhusianisha mafanikio yake na mimi. “Kaka, siku zote nakushukuru sana, japo huwa sikwambii, lakini wewe ndiye uliyenishauri na kunisaidia kuingia katika fani ya uandishi wa habari, nakushukuru sana,” alisema.

Furaha ile ilimfungua zaidi. Kama ilivyo kwa mwanadamu yeyote Yule, nilifurahi sana kwa utambuzi huo. Lakini lilikuwa fumbo. Hakika lilikuwa fumbo.

Tuliongea mawili matatu kuhusu mambo ya miongo miwili iliyopita na jinsi nilivyofanikiwa kumshawishi kubadili fani kutoka ualimu wa shule ya msingi hadi kuwa mwana habari mahiri, akitoka katika kufundisha darasa moja hadi kufundisha umma wa watanzania kupitia media.

Tulifurahi na kuahidi kukutana tena ili kuweka mikaka mipya ya maisha ya hapa duniani. Sikujua simu ile ndiyo ilikuwa ya mwisho kwetu kuongea katika uhai huu.

Sasa ndiyo ninaelewa kwa nini Roho wa Mungu alimwongoza Shadrack Sagati kukumbushia mambo yaliyotokea zaidi ya miongo miwili wakati akiingia katika fani ya uandishi wa habari. Sikujua kuwa alikuwa anatoa shukurani akijiandaa kuhitimisha safari yake katika dunia hii.

Mwenyezi Mungu alitupatia nafasi nzuri ya kuagana. Hapo ndipo ninaamini katika Roho wa Mungu ndani ya wanadamu. Mambo mengi yanaongozwa na Mungu pasipo sisi kufahamu. Hili ni mojawapo. Mimi nimejifunza.

Ni rahisi kusema kuwa maisha ya Sagati yamezimika mapema na ghafla kama mwanga wa mshumaa.

Hata hivyo Imempendeza Mwenyezi Mungu ameona heri kumpa pumziko mdogo wangu Sagati. Ameitwa na Bwana naye ameitika. Jina la Bwana lihimidiwe.

Tunapokuwa tunamshukuru sana Mungu kwa maisha ya utumishi ya Sagati, wakati mioyo ikijaa huzuri nyingi na machozi kuchuluzika machoni na mioyoni, tuinamishe vichwa kumshukuru Mungu kwa zawaji njema ya Sagati hapa duniani. Hata hivyo, mwisho bado.

Ni wakati kama huu, mioyo yetu inapojawa na huzuni kubwa, Elvis Presley, mwimbaji wa zamani wa Marekani alisema na anaeleza mustakabali wenye faraja kubwa…anaimba na kusema;

 *“si mbali sana tutafika mwisho wa safari ya maisha. Yawezekaza kamwe hatutakutana tena. Hadi tutakakusanyika katika jiji ling’aalo la mbinguni, kule mbali kabisa katika pwani ile nzuri sana.*

*Mahali ambapo maua huchanua milele zote bila kunyauka na kule hapatakuwa na kuagana tena. Kama hatutaonana tena katika ng’ambo hii ya mbingu, nitakutana na wewe katika pwani ile nzuri ya mbinguni.”*

LALA SALAMA MDOGO WANGU SHADRACK. USINGIZI MWEMA.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages