Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Uhusiano wa Nje wa Iran amesema kuwa, baada ya makundi ya kigaidi kushindwa huko Syria na Iraq sasa yanahamishiwa katika maeneo mengine hususan Afghanistan na kaskazini mwa Afrika.
Dakta Kamal Kharrazi amesema hayo katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Baraza la Saba la Kimataifa la Amani mjini Beijing China na kueleza kuwa, kujitolea kwa vikosi vya Iraq, Syria, Iran, Lebanon na wengineo kumepelekea kusambaratika kundi la kigaidi la Daesh, ingawa maktaba ya kifikra na uzalishaji wake bado vinaendelea kufanya kazi.
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Uhusiano wa Nje wa Iran amesema kuwa, kwa kuzingatia kwamba, katika stratejia ya usalama wa taifa ya Marekani, nchi kama China, Russia na Iran zinahesabiwa kuwa ni tishio, kuongezeka hatua za kigaidi za Daesh ni jambo ambalo linapaswa kutazamwa kwa umuhimu wa aina yake.
Dakta Kharrazi aidha amesema kuwa, chimbuko la fikra za makundi ya kuchupa mipaka ni Uwahabi unaonezwa na Saudi Arabia.
Waziri huyo wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema pia kuwa, viongozi wa Marekani wamekiri bayana juu ya nafasi ya nchi yao katika kuanzishwa makundi ya kigaidi likiwemo hili la Daesh, hatua ambayo ilitimia kwa kushirikiana Washington na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo hili la Mashariki ya Kati.
Mkutano wa Baraza la Saba la Kimataifa la Amani ulifanyika jana mjini Beijing China ukiwa na anwani ya "Usawa, Kutopendelea Upande Wowote na Uadilifu".
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇