Mahakama ya Afrika Kusini imeahirisha kwa mara nyingine tena kesi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Bwana Jacob Zuma na sasa itasikilizwa Novemba 30 mwaka huu.
Jacob Zuma anakabiliwa na kashfa ya rushwa katika mkataba wa silaha. Chanzo kimoja cha mahakama kimesema kuwa, kesi hiyo imeahirishwa ili kuwezesha wanasheria wake wapya kufahamu yaliyomo katika kesi inayomkabili mteja wao.
"Kesi yako imeahirishwa hadi Novemba 30, 2018," Jaji Mjabuliseni Madondo alimwambia mtuhumiwa, ambaye alikua amesimama kizimbani katika mahakama ya Pietermaritzburg, kaskazini mwa Afrika Kusini.
Jacob Zuma, mwenye umri wa miaka 76, anatuhumiwa kuwa alipokea rushwa kutoka kwa kampuni ya elektroniki na ulinzi Thales katika mkataba wa silaha wenye thamani ya karibu euro bilioni 4 uliotolewa mwaka 1999.
Jacob Zuma, ambaye alikuwa Rais wa Afrika Kusini kuanzia 2009 hadi Februari mwaka huu alipolazimika kujiuzuulu, amekanusha tuhuham hizo.
Mwanasheria wa "Kihistoria" wa Jacob Zuma, Michael Hulley, hivi karibuni alijiondoa kwenye kesi hiyo kwa sababu ya utata kuhusu malipo ya ada yanayohusiana na utaratibu wa mahakama kwa mteja wake ambayo yalitakiwa kulipwa na serikali.
Mwanasheria wake mpya amesema leo Ijumaa mbele ya mahakama kwamba, anatarajia kuwasilisha ombi la kufuta mashtaka dhidi ya Jacob Zuma lakini ametaka kupewa muda wa mwisho wa kujua undani wa mashitaka yanayomkabili.
Kesi ya Zuma inatambuliwa kuwa ni ya aina yake barani Afrika ambako ni mara chache sana kwa viongozi na wanasiasa wa vyama tawala kupandishwa kizimbani kwa tuhuma kama za ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇