Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Morogoro.
Mfumo ulioboreshwa wa
kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (PlanRep) unategemea
kuimarisha usalama wa nyaraka za Serikali kwa kuzihifadhi katika mtandao.
Hayo yamesemwa leo
Mkoani Morogoro na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Frank Jacob alipozungumza na
mwandishi wa habari hii juu ya umuhimu wa mafunzo yanayoendelea mkoani humo kwa
watumiaji wa mfumo huo.
Dkt. Jacob amesema
kuwa anaishukuru Serikali pamoja na wafadhili wa mradi huo kwa kuwaza
kuurekebisha mfumo huo na kuuboresha ili utumike katika sekta zote.
“Kwa kifupi mfumo
ulioboreshwa utakuwa na utunzaji wa nyaraka za Serikali wa hali ya juu kwa
sababu mwanzoni kila afisa husika wa kuandaa mipango na bajeti alikuwa akiandaa
taarifa hizo na kuzihifadhi katika kompyuta hivyo ikitokea imeharibika au
kuibiwa taarifa zote zinapotea lakini kwa sasa tutahifadhi moja kwa moja katika
mtandao ambao hauwezi kufuta au kupoteza taarifa yoyote”, alisema Dkt. Jacob.
Dkt. Jacob ameongeza
kuwa kuboreshwa kwa mfumo huo kutasaidia kurahisisha kazi kwa sababu kuna
taarifa nyingi hasa za takwimu zilikuwa zikiingizwa kwa njia za kawaida zinazotumia
muda mrefu lakini kupitia mfumo huo wataweza kuingiza takwimu hizo kiurahisi
kufuatia mfumo huo kuunganishwa na mifumo mbalimbali.
Vile vile kulikuwa na
changamoto ya kupishana kwa taarifa katika majumuisho kwani kila afisa husika
anafanya mahesabu ya taarifa zake kwa kutumia njia za kawaida ambazo kwa bahati
mbaya zinaweza zisifanywe kwa usahihi.
Aidha, Dkt. Jacob
amefafanua kuwa kupitia mfumo huo Wizara itaboresha utendaji kazi na
itawajengea uwezo Mikoa kufanyia kazi changamoto za Halmashauri kwa sababu
mfumo huo hautaruhusu taarifa za Halmashauri kwenda Wizara husika moja kwa moja
bila kupitia mkoani.
Mfumo huo mpya wa
kitaifa umeboreshwa kwa ajili ya kutumika katika sekta zote za umma na umehuishwa
na mifumo mingine ya Serikali ili kuboresha usimamizi na kuiwezesha Serikali
katika ngazi zote kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa
jamii.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇