Washiriki wa warsha ya siku
mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni za Taarifa
za Usafirishaji na uingizaji wa fedha tasilimu kutoka na kwenda nje ya nchi
wakifuatilia kwa makini mjadala katika warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi
wa Benki Kuu (BoT) jijini Dar es Salaam.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa Kanuni za
taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na kwenda nje ya
nchi (Crossborder Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instruments
Regulations) ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na wasafiri wote wanaotoka
au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha taslimu wanazosafirisha
ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola za kimarekani elfu kumi
(USD 10,000).
Akizungumza wakati
wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni hizo,
Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) Ndugu
Onesmo H. Makombe alisema utekelezaji wa kanuni hizi, pamoja na mambo mengine
utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.
“Takwimu hizo zitakazosaidia
pamoja na mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji
na kuhakikisha kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha
zitokanazo na uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi” alisema Bw.
Makombe
Aidha kanuni hizo zimeweka adhabu zitakazochukuliwa
dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha zinazolingana au zinazozidi
kiwango kilichowekwa bila kutoa taarifa
au watakaotoa taarifa za uongo.
Alizitaja adhabu hizo kuwa ni pamoja na
kukamatwa kwa fedha taslimu walizonazo na kuchukuliwa hatua nyingine za
kisheria kama vile kufunguliwa mashtaka.
“Wahalifu pamoja na
mambo mengine, wanapenda kusafiri na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia
benki kutuma fedha kutokana na umakini unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza
kuwepo mipakani” Alisisitiza Bw. Makombe
Kamishna
huyo
amewaasa washiriki wa warsha hiyo kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu
na uaminifu mkubwa ili kuziba mianya yote ambayo wahalifu
wanaweza kuitumia kutimiza kusudi lao ovu na kuhatarisha usalama wa
nchi.
Kutokana na umuhimu
wa ushiriki wa wadau mbalimbali katika utekelezaji wa kanuni hizo warsha hiyo
imejumuisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali wengi wao wakiwa ni maafisa
forodha.
Washiriki hao
wametoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Wizara ya Mambo
ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kikanda, Mamlaka ya Mapato Tanzania na vikosi vya ulinzi na usalama
Wengine ni Bodi ya
Mapato Zanzibar, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo-Zanzibar, Shirika la Posta, Benki kuu ya Tanzania, Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashitaka-Zanzibar, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka-Tanzania Bara Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania Bara na Zanzibar, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Idara ya uhamiaji na Kitengo cha Kudhibiti
Fedha Haramu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇