NA BASHIR NKOROMO
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori amesema, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, itahakikisha inamaliza migogoro ya ardhi iliyopo sasa na kuhakikisha hakuna mipya itakayotokea tena katika Manispaa hiyo.
Amesema kufuatia hatua inazochukua Halmashauri hiyo, migogoro ya ardhi iliyokuwepo sasa imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kushughulikiwa na uongozi, na hatua iliyobaki ni kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika kabisa kwa kuwa ni miongoni mwa kero kubwa kwa wananchi.
Makori alisema hayo, baada ya kufungua semina ya siku nne ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa Kata na Mitaa jana, katika ukumbi wa Manispaa ya Ubungo, ambayo ilihusu kuwapa weledi viongozi hao kufahamu vema sheria za ardhi, mwongozo mpya wa mapokezi na matumizi ya fedha za Serikai kwa ajili ya maendeleo ya serikali za mitaa (LGDG),Mpango wa fursa na vikwazo kwa maendeleo,Rushwa mahala pa kazi, Ulinzi na Usalama.
Alisema, moja ya sababu ambazo zimebainika kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi katika manispaa hiyo, ni uelewa mdogo wa baadhi ya viongozi na wananchi kuhusu sheria za ardhi hali ambayo imetoa mwanya kwa matapeli kuitumia kujinufaisha kinyume cha sheria.
"Unakuta katika mgogoro fulani wa ardhi viongozi ambao ndio wangesaidia kuutatua kumbe nao ni sehemu na chanzo cha mgogoro huo kwa kushiriki moja kwa moja au kwa kudanganywa na matapeli, sasa semina kama hii ni miongoni mwa mbinu tunazotumia kuhakikisha migogoro ya ardhi inakwisha katika Halmashauri yetu", alisema Makori.
Makori alisema, mafunzo katika semina hiyo yatahusu pia masuala ya Utawala Bora, Majukumu ya Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa Kata na Mitaa, Pia kujifunza kuhusu historia na uhalali wa serikali za Mitaa, Sheria za uendeshaji wa Mamlaka za serikali za Mitaa, Muundo, Madaraka na Majukumu ya serikali za Mitaa, Mamlaka za serikali za Mitaa, Maadili ya viongozi wa Umma na Ulinzi na usalama katika maeneo ya kazi.
Akifungua semina hiyo, Makori alisema, ina lengo pia la utekelezaji wa mpango wa mafunzo ulioidhinishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Makori alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Dk. John Kayombo kwa kuandaa semina hiyo, akisema kuwa imetoa fursa kwa Wenyeviti na Watendaji wa Kata na Mitaa kuimarika katika nidhamu ya utendaji hususani kutekeleza mambo yaliyoainishwa kutekelezwa katika maeneo yao kwa maslahi ya wananchi.
Alisema kuwa mafunzo hayo yatatoa ufanisi wa uelewa mipaka na mamlaka katika utendaji jambo ambalo litawasaidia kuepuka migongano ya kimaslahi katika utekelezaji wa shughuli za uwakilishi wa wananchi pamoja na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Halmashauri.
Makori alisema mada zote ziatakazotolewa zitakuwa ni chachu ya kufungua ukurasa mpya kwa kuzingatia misingi ya utawala bora kwa kufuata miiko ya uongozi na kuongeza uadilifu katika utendaji kazi wa kila siku ili kufikia malengo yaliyoidhinishwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Kayombo alisema kuwa lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo katika kutatua matatizo ya wananchi, kuwasilisha mawazo yao katika vikao vya kisheria, kuchambua sera na mikakati ya kutekeleza mipango mbalimbali, kutafuta ufumbuzi wa changamoto za wananchi katika maeneo yetu ya kusimamia majukumu yetu kikamilifu.
Kayombo alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuinua kiwango cha utendaji kazi kwa kuongeza stadi na maarifa ya uongozi ambayo yatachangia kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao ikiwa ni pamoja na kuondoa migogoro ya kila siku baina ya Wenyeviti wa Mitaa na Watendaji wa Kata na Mitaa.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori akifungua Semina ya siku nne ya kuwajengea weledi Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa Kata na Mitaa, katika Ukumbi wa Manispaa ya Ubungo, Kibamba, Dar es Salaam, jana. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo James Mkumbolia na Kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo John Kayombo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo John Kayombo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo James Mkumbolia na Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo John Kayombo wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo.
Washiriki wakiwa kwenye ufunguzi wa semina hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake baada ya kufungua Semina hiyo leo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo John Kayombo akionyesha kipeperushi kilichoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa hiyo, kwa ajili ya elimu kwa wananchi kuhusu ulipaji kodi na mipango mingine ya maedeleo kwa mwaka 2017/18. PICHA: BASHIR NKOROMO
Your Ad Spot
Jun 21, 2017
Home
Unlabelled
MANISPAA YA UBUNGO YAJIKITA KATIKA KUKOMESHA MIGOGORO YA ARDHI
MANISPAA YA UBUNGO YAJIKITA KATIKA KUKOMESHA MIGOGORO YA ARDHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇