FIDEL CASTRO |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, amemtumia salamu
za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Raul Castro kufuatia kifo cha Rais
Mstaafu wa Cuba Mhe. Fidel Castro kilichotokea tarehe 25 Novemba, 2016.
Katika
Salamu hizo Rais Magufuli amesema;
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa za kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Fidel Castro. Kwa
niaba ya Serikali, Wananchi wa Tanzania na kwa niaba yangu mwenyewe natoa pole
nyingi kwako, familia, Serikali ya Cuba na wananchi wa Cuba kwa kumpoteza mtu
muhimu.
Fidel Castro alikuwa kiongozi shupavu
wa karne, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika ukombozi wa nchi za Kusini
mwa Afrika na pia kwa misaada mikubwa aliyoitoa katika kuboresha huduma za
kijamii kwa wananchi.
Alikuwa rafiki wa Tanzania na Afrika
nzima, historia ya Tanzania na Afrika haziwezi kukamilika bila kumtaja Fidel
Castro, hakika kifo chake sio tu ni pigo kwa Cuba bali pia kwa Tanzania na
Afrika.
Naungana nawe na wananchi wa Cuba
katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, na pia nakuombea kwa Mwenyezi Mungu
wewe, familia na wananchi wote wa Cuba muwe na nguvu, subira na ustahimilivu
kutokana na kuondokewa na mpendwa wenu."
Pia
Rais Magufuli amemuombea marehemu Fidel Castro apumzishwe mahali pema peponi,
Amina.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇