Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) Dkt. Donald Kaberuka mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu
jijini Dar es Salaam. Picha na IKULU
HABARI KAMILI
HABARI KAMILI
Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Wataalamu huru lililoundwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kuangalia mahusiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wadau wa Maendeleo Dkt. Donald Kaberuka, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika Mazungumzo hayo Rais Magufuli amemshukuru Dkt. Kaberuka kwa mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa kipindi chake cha uongozi wa Benki ya AfDB ambapo Tanzania ilipata ushirikiano mzuri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ujenzi wa barabara.
Dkt. Magufuli amesema anaamini kuwa Dkt. Kaberuka ataendelea kutoa ushauri mzuri kwa Tanzania katika juhudi zake za maendeleo ikiwemo ushauri utakaotolewa katika ripoti ya jopo analiloongoza kuhusu mahusiano ya Tanzania na wadau wa maendeleo.
"Tanzania itaendelea kushirikiana na wewe na tunaamini kuwa unayo nafasi ya kutushauri katika mipango yetu mbalimbali ya maendeleo, kama vile namna tunavyoweza kunufaika na rasilimali nyingi tulizonazo yakiwemo madini mbalimbali, gesi asilia, ardhi kubwa, mifugo mingi hususani ng'ombe, bandari, maziwa na bahari na mbuga za wanyama" Amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Dkt. Donald Kaberuka pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano amesema hatua zilizoanza kuchukuliwa na serikali yake katika kuimarisha ukusanyaji wa kodi, kukabiliana na rushwa na mipango ya kutumia rasilimali zilizopo ipasavyo zinaonesha Tanzania inaelekea kupiga hatua nzuri za kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇