LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 13, 2013

UMOJA WA MATAIFA WAIDHINISHA UJENZI WA MAJENGO YA TAASISI YA KIMATAIFA -TANZANIA

NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa    limepitisha  kwa kauli moja Azimio  linalopendekeza kuidhinishwa  kwa hatua zote za   Ujenzi wa  Mradi wa   Taasisi mpya ya Kimataifa  itakayochukua  majukumu  ya   Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR).

Mradi huo wa majengo ya  kisasa, utajengwa katika eneo la LakiLaki Jijini Arusha-Tanzania na   utahusisha Ofisi, vyumba vya  mahakama, na sehemu ya kutunzia nyaraka na kumbukumbu zote za  ICTR.  Eneo hilo la Laki Laki limetolewa na Serikali ya Tanzania kwa Umoja wa Mataifa.

 Baraza    Kuu limepitisha Azimio hilo katika  mkutano wake uliofanyika siku ya Ijumaa ( April 12),mkutano ambao  pia, Baraza lilipokea na kupitisha  maazimio mengine Nane  yaliyowasilishwa na  Kamati ya Tano inayohusika na masuala ya  Utawala na Bajeti katika Umoja wa Mataifa.

Taasisi hiyo mpya  ijukulikanayo kama  Mfumo wa Kimataifa wa Kumalizia  Mashauri Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya  Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari au kwa kimombo (  International Residual Mechanism for Criminal Tribunal )- Tawi la Arusha   pamoja na kuhifadhi nyaraka itasimamia kesi za Masalia ambazo zitakuwa bado hazijakamilia baada ya  ICTR kumaliza muda wake mwakani.

Azimio hilo pamoja na mambo mengine, linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuweka bayana uwajibikaji na uangalizi wa kina katika ujenzi wa mradi ikiwa  ni pamoja na  kuhakikisha kwamba, sheria, taratibu, kanuni na miongozo yote ya  Umoja wa Mataifa     inayohusu manunuzi/ugavi inafuatwa  ipasavyo katika utekelezaji wa mradi huu.

Gharama za mradi zinatarajiwa kuwa kiasi cha dola za kimarekani 8.78 Milioni ( takribani  Sh.14 Bilioni). Fedha hizi zinalipwa na  Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Mradi unatarajiwa kukamilika  kabla ya mwishoni mwa  mwaka 2015.

Aidha kupitia Azimio hilo,  Baraza Kuu  pia limeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea na jukumu la  kufuatilia kwa karibu mchakato wote unaohusiana na  utekelezaji wa mradi na vilevile katika kuhakikisha kwamba  inashirikiana na Umoja wa Mataifa kufanikisha  Mradi huu.

Halikadharika  kupitia  Azimio hilo, Baraza Kuu limeelezea  kufurahishwa na  maendeleo ya utekelezaji wa mradi hasa kwa kutumia ujuzi wa ndani, (Local knowledge) katika  ubunifu wa majengo (design),   upatikanaji wa  meneja wa mradi na maandalizi ya kina ya gharama za  ujenzi.

Pamoja na pendekezo la  kuidhinishwa kwa hatua za ujenzi wa mradi ,  Baraza pia  kupitia  Azimio hilo , linamtaka KatibuMkuu   kufanya juhudi zote zitakazo pelekea  kupunguza muda wa ujenzi wa mradi .

Katika hatua nyingine,  Baraza  Kuu pia linamtaka Katibu Mkuu  kuanza mazungumzo na Asasi nyingine za Kimataifa ikiwamo ile ya Mahakama Afrika itakayoshughulikia   Haki za Binadamu,  juu ya namna bora ya  kushirikiana katika matumizi ya  miundo mbinu hiyo katika siku za usoni.

Mwaka 2010 Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Azimio nambari  1966  la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa utakaomalizia Mashauri ya Masalia  kwa zilizokuwa   Mahakama za Kimataifa za Mauaji ya Kimbari  yaliyotokea  nchini Rwanda ( ICTR) na Mauaji ya  halaiki yaliyotokea katika  iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani ( ICTY).

Katika azimio hilo Baraza Kuu la Usalama lilibainisha wazi  kwamba  Arusha ndiyo itakuwa makao ya  Tawi la mfuno huo mpya na  The Hague ikiwa ni  makao ya Tawi  jingine.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages