LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 31, 2020

SHUKRANI JPM KWA UAMUZI MGUMU, LAKINI ULIOJAA BUSARA KUIWEKA TZ TULIVU KUHUSU KORONA


MKUU wangu wa Nchi, nimeamua kukushukuru kwa uamuzi  wako Mgumu wenye Busara wa kuwataka Watanzania waache kutishana kuhusu ugonjwa wa Corona, bali waendelee kuchapa kazi, lakini kwa tahadhari kubwa juu ya Ugonjwa huo hatari uliozikumba nchi masikini na tajiri duniani.

Wakati unatoa uamuzi huo hukukurupuka kwa kuiga marufuku zinazotolewa na viongozi wa nchi mbalimbali, za kuwataka wananchi wao wasitoke nje kwa siku kadhaa wakidhani ndo njia mojawapo ya  kuudhibiti ugonjwa huo , bali wewe ulitulia na kufikiria mazingira ya nchi yako na hali halisi ya maisha ya Watanzania.

JPM,ulijua kabisa kwamba ukikurupuka na kuwaiga viongozi wenzako, licha ya uchumi kuyumba, bali kwa kiasi kikubwa ungewaumiza wananchi wa hali ya chini walio wengi ambao bila kutoka kutafuta  hawawezi kupata mlo wao wa siku.

Pia, hali ya nchi ingevurugika kama tunavyoshuhudia  kila kukicha vurugu katika Nchi jirani na mataifa mengine makubwa, ambako wananchi wameshindwa kuhimili/kuvumilia njaa na mateso wanayopata na familia zao  baada ya kukosa mahitaji yao muhimu kwa katazo la kutotoka majumbani.Lakini pamoja na amri hizo idadi ya wagonjwa inazidi kuongezeka.

Tumekuwa tukishuhudia mapambano kati ya raia na askari wakiwapiga viboko na mabomu ya machozi waliokiuka amri ya kukaa majumbani, lakini si kwa kupenda bali wamelazimika kutoka kwenda kutafuta riziki baada ya kukabwa na njaa kali. Je, hilo ndo suluhisho?

Rais wetu, uamuzi wako huo mgumu, umeliepusha Taifa na mambo mengi  mabaya ambayo yangetokea  endapo ungewaiga marais wenzako. Kuna haja hata ya marais hao kukuiga wewe ili kuleta utulivu katika nchi zao.

JPM,huwa nakaa na kufikiria endapo ungetoa amri ya Watanzania kutotoka nje, hivi ingekuwaje? Kwanza hali hii tu ya tahadhari ya korona, imeshatuvuruga na kuvuruga uchumi, ikiwemo ya kukosa watalii ambao wanaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni, baadhi ya mahoteli  yamefungwa kwa kukosa wateja.

Hali hiyo, imesababisha wafanyakazi kupunguzwa na hata wengine kuachishwa kazi. Kampuni zilizokuwa zinasambaza vyakula na huduma zingine kwenye hoteli hizo zimekosa kazi. Ndege zimekosa abiria na biashara kwa ujumla kuyumba.

Kampuni na wafanyabiashara waliokuwa wameingia mikataba na shule/ vyuo ya kusambaza vyakula  na mahitaji mengine hivi sasa hawana kazi.

Orodha hiyo ni mifano michache tu, lakini watu wengi wameathirika kwa katazo hilo dogo la kupunguza misongamano ambayo ni hatari kwa maambukizi ya Korona ambayo hadi sasa haina kinga wala tiba.

Watanzania wangepigwa marufuku kutoka nje mambo mengi mabaya yangetokea; Wengi wa walalahoi hasa walioko mijini wangeshindwa kuvumilia, bila kupenda wangetoka kwenda kutafuta riziki bila kujali kupigwa na askari.

Hali ingewazidia wangekwenda kuvamia maduka ya vyakula kwa kupora kwani hata fedha za kununulia wangekuwa hawana. Baada ya maduka kuishiwa vyakula wangeanza kuvamia nyumba za watu wenye ahueni kimaisha na kupora chochote walicho nacho.

JPM, hali ingekuwa hatari zaidi, tungeanza kuporana wenyewe kwa wenyewe mitaani. Sidhani kama majeshi yetu yangeweza kutuliza ghasia hizo, kwani ni dhahiri idadi ya askari wa majeshi yetu ni chache sana kuliko wingi wa wananchi, wangezidiwa tu.

Isitoshe ungezuka uhasama mkubwa kati ya wananchi na askari. Hatari zaidi ingekuwa kwa askari wanaoishi na familia zao uraiani, wangefanyiwa vurugu kulipiza kisasi. Nakushukru sana JPM kwa uamuzi wako huo mgumu umeepusha mengi.

Na endapo raia wangetii amri ya kutotoka majumbani, basi, walalahoi wasio na chochote wala akiba ya vyakula, wangekufa wengi kwa njaa, vifo ambavyo vingekuwa vingi kuliko vifo vya korona vinavyotokea kwa sasa Italia na Marekani. Nasema kinachotakiwa ni kumuunga mkono JPM kwa hali na mali kkwa kuwa na tahadhari kubwa na ugonjwa huo.

Lakini vile vile tujiulize, hivi Serikali yetu ina uwezo wa kuwasambazia chakula na mahitaji mengine wananchi wakibaki majumbani?

JPM, kwa uamuzi huo mgumu. Umeepusha kundi kubwa la raia wasio kuwa na ajira kama vile; waendesha Bodaboda, mama/baba  lishe, machinga, vibarua  na baadhi ya wakulima wadogo wadogo wanaotegemea kuuza mazao yao ndiyo wapate mlo wa siku. Hivi kundi hilo na familia zao lingeingia barabarani kutafuta riziki ya mlo wa siku, askari wetu wangeweza kulizuia?!!!

Pia, nawachukiana kupingana nao baadhi ya Watanzania walioko nje ya nchi na ndani ya nchi ambao wanaubeza uamuzi wako, wakitaka uige uamuzi wa unaotolewa na baadhi ya marais katika nchi zao wa kupiga marufuku wananchi kutoka majumbani kwa siku kadhaa kwamba ndiyo njia muafaka ya kupambana na Korona.

Naamini,wengi hawajui mazingira ya nchi yetu, wanayafananisha na huko waliko. Na waliopo nchini nao hawajui ipasavyo mazingira yetu na endapo amri hiyo ikifuatwa hawajui athari ambazo zingetokea.

JPM, nakushukuru wewe na Mwenyezi Mungu aliyekuongoza kutoa uamuzi huo mgumu wenye busara. Kinachotakiwa kwa Watanzania ni kumuunga mkono kwa Rais Wetu, kwa kufuata maagizo na maelekezo ya Serikali, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  jinsi ya kupambana na ugonjwa huo hatari.

JPM, pia nashauri Serikali yetu iendelee kuwa na msimamo wa kulinda mipaka yetu, na njia zote za panya kuwabaini wageni wote waingiao nchini kwa kuwapima joto (Korona) na kuwaweka eneo la uangalizi kwa siku 14. Jambo hilo lisiwe na chembechembe zozote za upendeleo/ubaguzi, awe raia, si raia au kiongozi yeyote, wote wapimwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

JPM, kila siku namuomba Mungu atuepushe na gonjwa hili la hatari lisiendelee kusambaa nchini. Na ifikapo Aprili 17, mwaka huu, siku ambayo tunatimiza mwezi mmoja tangu utoe uamuzi huo mgumu, Mungu akuongoze tena kwa kutoa uamuzi wenye faraja kwa Watanzania, ili ikiwezekana hata shule na vyuo vifunguliwe pamoja na mikusanyiko mingine irudi kama kawaida.

Lakini tutafikia hapo kwa watanzania kumuunga mkono Rais wetu katika mapambano ya kuutokomeza ugonjwa huo. Tusipofanya hivyo,  basi tusije tukamlaumu JPM kwa atayoyatangaza  siku hiyo.



Ndimi, Richard Mwaikenda
Senior Photojournalist
0754264203
Ukonga, Dar es Salaam.
March 31,2020.



1 comment:

  1. Mimi naunga mkono busara za Rais wetu mpendwa kutofunga kabisa shughuli za kila siku bali kuchukua tahadhari ya hali ya juu.Ushauri wangu ili tuweze kuwa salama tufunge kwa muda wageni kuingia nchini kwani mataifa mengine idadi ya wagonjwa ni ya kutisha.Tusipo zuia tutajikuta wameingia wengi hata tukija kuzuia tutakua tumechelewa

    ReplyDelete

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages