LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 23, 2026

WABUNGE WAPIGWA MSASA MABORESHO YA eRITA

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Edwin Swale, amesema wajumbe wa kamati hiyo wamepata uelewa kuhusu maboresho ya mfumo wa kielektroniki wa eRITA yanayolenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kupunguza urasimu.

Swale, ambaye pia ni Mbunge wa Lupembe mkoani Njombe, ameeleza hayo baada ya kikao na uongozi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kilichofanyika Oktoba 22, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Bunge jijini Dodoma.

Amesema maelezo yaliyotolewa na RITA yamewapa wajumbe fursa ya kuelewa namna mfumo huo unavyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa kupunguza muda wa kusubiri, gharama na taratibu zisizo za lazima.

Kupitia eRITA, wananchi wanaweza kuwasilisha maombi, kuhakiki taarifa na nyaraka, kufanya malipo na kufuatilia uchakataji wa maombi yao hadi kupata huduma au nyaraka husika.

Huduma zinazotolewa kupitia mfumo huo ni pamoja na usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa, vifo, ndoa na talaka, pamoja na huduma zinazohusiana na bodi za wadhamini.

Miongoni mwa maboresho yaliyofanyika ni kuwezesha uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kwa njia ya kielektroniki, malipo kwa kutumia kadi za benki na kufanya marekebisho ya vyeti kupitia mfumo huo.

Aidha, wananchi wanaweza kupata taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika kushughulikia maombi yao kupitia ujumbe wa simu au akaunti zao za mfumo, hatua inayorahisisha ufuatiliaji bila kulazimika kufika ofisini mara kwa mara.

HUDUMA ZAIDI KWA NJIA YA KIDIJITALI
Maboresho hayo yameongeza fursa kwa wananchi kupata huduma za RITA wakiwa ndani au nje ya nchi, huku yakisaidia kupunguza gharama za usafiri na muda unaotumika kufuatilia maombi.

Matumizi ya mfumo huo pia yanalenga kuimarisha ubadilishanaji wa taarifa kati ya taasisi za Serikali na sekta binafsi, kurahisisha upatikanaji wa kumbukumbu na kuboresha ufanisi katika utoaji wa huduma.

Kwa mujibu wa maelezo ya RITA, matumizi ya eRITA yamechangia kuimarisha usalama wa kumbukumbu, uwazi na uwajibikaji, sambamba na kupunguza utegemezi wa mifumo ya karatasi.

Mfumo huo pia unaiwezesha taasisi hiyo kupata takwimu muhimu zinazoweza kutumika katika kupanga na kufanya maamuzi kuhusu utoaji wa huduma kwa umma.

RITA YATAJA MAFANIKIO YA TEHAMA

Katika hatua nyingine, RITA imeeleza kuwa imepata tuzo ya Mradi Bora wa TEHAMA katika Sekta ya Umma, katika kipengele cha kupunguza urasimu.

Pia, katika mwaka wa fedha 2025/2026, taasisi hiyo iliingia katika orodha ya taasisi 10 bora zilizofanya maboresho katika matumizi ya mifumo ya kidijitali na utoaji wa huduma.

RITA imeahidi kuendelea kuboresha mfumo wa eRITA kwa kuwekeza katika miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kuimarisha usalama wa taarifa na kutoa mafunzo kwa watumishi wake.

Taasisi hiyo pia imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo huo ili kuongeza uelewa na kuwahamasisha wengi zaidi kutumia huduma za kielektroniki.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mbunge wa Lupembe, Edwin Swale akiongoza kikao kati ya wajumbe wa wa kamati hiyo na uongozi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) uliowasilisha  maboresha ya utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia mfumo huo wa kielektroniki wa eRITA.

Viongozi wa RITA wakijitambulisha katika kikao hicho.










 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages