Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Kichiki Lugangira, ametoa maelekezo kwa viongozi wa Wilaya, halmashauri na wataalamu wa afya kwa ngazi zote Mkoa wa Arusha kuhakikisha Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatekelezwa kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji ili kuwafikia wananchi wote wanaohitaji huduma za afya.
Maelekezo hayo ameyatoa leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, wakati akizindua awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote mkoani Arusha, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, katika viwanja vya Field Force Unity (FFU), Kwa Mrombo, jijini Arusha, akisema ni muhimu kwa Viongozi wa ngazi zote kuhakikisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatafsiriwa katika huduma halisi zinazomfikia mwananchi wa kawaida.
Mhe. Lugangira amesema viongozi wanapaswa kuhakikisha mpango huo unawafikia wananchi wote, wakiwemo wakulima, wafugaji, wafanyabiashara wadogo, waendesha bodaboda, vijana, wazee na wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Amesisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote inalenga kulinda familia dhidi ya gharama kubwa za matibabu, kupunguza umasikini unaotokana na maradhi na kuhakikisha wananchi hawalazimiki kuuza mali zao au kukopa fedha ili kupata huduma za afya.
Aidha, amewataka viongozi na watendaji kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinakuwa tayari kuwahudumia wananchi, mifumo ya ndani ya udhibiti inafanya kazi na malalamiko yanayowasilishwa yanashughulikiwa kwa wakati.
Mhe. Lugangira ameongeza kusema kuwa mafanikio ya mpango wa Bima ya afya kwa wote hayatapimwa kwa idadi ya wananchi walioandikishwa pekee, bali pia kwa ubora wa huduma zinazotolewa, namna wananchi wanavyopata huduma wanazohitaji na imani inayojengwa kati ya Serikali na wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Arusha Bw. Hipoliti Lello amebainisha kuwa serikali imeweka kipaumbele kwa kaya zisizo na uwezo ambapo kwa Mkoa wamelenga kusajili Kaya 29, 334 zenye jumla ya wanufaika 80, 909 ambazo Kaya hizo zitalipiwa na serikali.




No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇