Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe CPA Amos Makalla, amewataka viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili lidumishe amani, mshikamano na usalama, huku wakishiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Lugangira ameyasema hayo leo, Oktoba 24, 2026, katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wakati wa kilele cha maombi ya kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuiepusha nchi na athari za mvua za El Niño. Amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kulinda amani na kuzingatia misingi ya umoja na mshikamano iliyowekwa na viongozi na wazee waliotangulia.
Amesema ni muhimu kwa wananchi kuendelea kulinda tunu za Taifa, kudumisha umoja na kuelekeza nguvu zao katika shughuli za maendeleo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, hususan vinavyowalenga wanawake na watoto katika Mkoa wa Arusha. Amewataka viongozi wa dini, viongozi wa kimila, viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla kushirikiana katika kuzuia vitendo hivyo, kutoa elimu kwa jamii na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi vinapotokea.
Ameeleza kuwa kulinda haki, utu na usalama wa wanawake na watoto ni sehemu muhimu ya kujenga jamii yenye amani, upendo na mshikamano. Hivyo, amehimiza jamii kutofumbia macho vitendo vya ukatili na badala yake kushirikiana katika kuhakikisha waathirika wanapata msaada na hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya vitendo hivyo.
Vilevile, ameeleza kuwa amani, mshikamano na usalama ni nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa, kwani huwezesha wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii zinazochochea ustawi wa jamii.
Amewataka viongozi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia umoja, ushirikiano na maslahi mapana ya Taifa ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye amani, utulivu, maendeleo na ukuaji wa kiuchumi.




No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇