LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 18, 2026

WANAOCHEZEA VIPIMO KUKIONA CHA MTEMA KUN

 Na Richard Mwaikenda, Dodoma

Wakala wa Vipimo Nchini (WMA) umeweka wazi kuwa wafanyabiashara wanaochezea vipimo kwa kutumia mizani isiyo sahihi au kuuza bidhaa kwa vipimo visivyokidhi viwango wanakabiliwa na adhabu kali, ikiwemo faini inayoweza kufikia Sh milioni 100 na kifungo cha hadi miaka miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 18, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Mtumba jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, amesema sheria imeweka viwango tofauti vya adhabu kulingana na aina na marudio ya kosa.

Kihulla amesema mtuhumiwa anayekubali kosa anaweza kutozwa faini ya kati ya Sh100,000 na Sh20 milioni kwa kosa moja, wakati anayekana kosa na baadaye kupatikana na hatia mahakamani anaweza kutozwa faini ya Sh300,000 hadi Sh50 milioni, au faini pamoja na kifungo kisichozidi miaka miwili.

Amesema kwa mkosaji wa mara kwa mara, adhabu huwa kubwa zaidi, ambapo faini inaweza kufikia kati ya Sh500,000 na Sh100 milioni kwa kosa moja.

Kwa mujibu wa Kihulla, hatua hizo zinalenga kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia matumizi ya vipimo sahihi na kulinda haki za walaji dhidi ya kupata bidhaa pungufu ya kiasi walicholipia.

WANANCHI WATAKIWA KUDADISI

Kihulla amewataka wananchi kutokuwa watazamaji katika suala la usahihi wa vipimo, bali kuhakikisha wanadai kupimiwa kwa mizani na kutoa taarifa pale wanapobaini au kuhisi kuwa kipimo kilichotumika si sahihi.

Amesema WMA ina wajibu wa kuhakikisha kilo moja inakuwa kilo moja na kwamba vipimo vinavyotumika nchini vinaendana na viwango vinavyotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.

Aidha, amesema kazi ya WMA haiishii katika kusimamia vipimo vya bidhaa sokoni, bali inahusisha sekta mbalimbali zinazotegemea vipimo sahihi.

Ametoa mfano wa sekta ya afya, ambako vipimo vya uzito hukaguliwa ili kuhakikisha mgonjwa anapata uzito halisi, jambo linaloweza kumsaidia daktari kufanya uamuzi sahihi kuhusu kiwango cha dawa kinacholingana na uzito wa mgonjwa.


WMA YATOA NAMBA YA MALALAMIKO

Kihulla amewataka wananchi kushirikiana na WMA katika kupambana na matumizi ya vipimo visivyo sahihi kwa kutoa taarifa wanapobaini ukiukwaji.

Amesema wananchi wanaweza kuwasiliana na WMA kupitia namba 08001197 kutoa taarifa kuhusu vipimo vinavyotiliwa shaka ili hatua stahiki zichukuliwe.

Amesisitiza kuwa usahihi wa vipimo ni suala la kulinda haki za wafanyabiashara na walaji, huku akiwataka wote kuhakikisha biashara inafanyika kwa vipimo vinavyotambulika na vinavyoweza kuthibitishwa




.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages