LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 24, 2026

UJENZI UWANJA WA NDEGE MSALATO WAFIKIA ASLIMIA 89, KUKAMILIKA DESEMBA

 Na Richard Mwaikenda, Dodoma

UJENZI wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 30, 2026, huku kazi za miundombinu zikifikia asilimia 89.02 na majengo asilimia 78.37.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu hatua za mwisho za ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Amesema ujenzi wa miundombinu, unaotekelezwa kupitia Package 1, unatarajiwa kukamilika Novemba 27, 2026, wakati Package 2, inayohusu ujenzi wa majengo, inatarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026.

Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo na kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga katika ngazi ya kitaifa na kikanda.

RUNWAY YAFIKIA ASILIMIA 98

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji hadi Septemba 23, 2026, ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege umefikia asilimia 98, huku njia za kuunganisha ndege (taxiways) zikifikia asilimia 99 na eneo la maegesho ya ndege (apron) likifikia asilimia 99.

Kazi nyingine za Package 1 zimefikia hatua mbalimbali, zikiwemo barabara ya kuingia uwanjani, barabara za ndani na maegesho ya magari kwa asilimia 75; mfumo wa maji asilimia 89; uzio na mageti asilimia 76; pamoja na kazi za umeme na vifaa vya kuongozea ndege asilimia 90.

Kazi zilizobaki ni pamoja na upandaji wa nyasi katika maeneo ya usalama ya runway na taxiways, ufungaji wa taa za kuongozea ndege na barabarani, mabomba na tanki la maji la chini ya ardhi, ukamilishaji wa uzio na mageti pamoja na ufungaji wa mifumo ya mawasiliano ya ndege ikiwemo ILS na DVOR.

MAJENGO YAFIKIA ASILIMIA 78.37

Kwa upande wa Package 2, ujenzi wa majengo umefikia asilimia 78.37.

Jengo la abiria limefikia asilimia 81, Mnara wa Kuongozea Ndege asilimia 74, Kituo cha Huduma za Zimamoto asilimia 88, kituo kikubwa na vituo vidogo vya umeme asilimia 71, huku jengo la huduma za hali ya hewa (MTO) likifikia asilimia 87.

Kazi zinazoendelea ni pamoja na umaliziaji wa majengo, ufungaji wa mifumo ya mitambo, umeme na mabomba, mifumo ya TEHAMA na mawasiliano, mashine za ukaguzi wa mizigo, madaraja ya kupitishia abiria kwenye ndege (Passenger Boarding Bridges), vifaa vya hali ya hewa na magari ya zimamoto.

BOEING 787 KUTUA MSALATO

Katika awamu ya kwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unajengwa kwa hadhi ya Daraja la 4E, kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).

Uwanja huo utakuwa na runway yenye urefu wa mita 3,600 na upana wa mita 45, pamoja na mabega yenye upana wa mita 7.5 kila upande.

Miundombinu hiyo imeandaliwa kuwezesha uwanja kuhudumia ndege kubwa, ikiwemo Boeing 787 Dreamliner, yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 350.

Uwanja pia unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria takribani milioni 1.5 kwa mwaka na utawekewa mifumo itakayowezesha ndege kutua na kuruka mchana na usiku, katika misimu mbalimbali ya mwaka.

AJIRA 9,059 ZATOLEWA

Mradi huo pia umeendelea kutoa fursa za ajira kwa Watanzania, ambapo jumla ya ajira 9,059 zimetolewa katika kipindi chote cha utekelezaji.

Kati ya hizo, ajira 3,571 zimetolewa kupitia Package 1, huku Package 2 ikitoa ajira 5,488.

Aidha, jumla ya wafanyakazi 47 wa kigeni wameshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.

FURSA KUBWA KWA BIASHARA

Besta amewataka Watanzania, hususan wakazi wa Dodoma, kutumia fursa zitakazotokana na uwepo wa uwanja huo kukuza biashara zao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amesema uwanja huo unatarajiwa kufungua fursa katika biashara zinazohitaji usafirishaji wa haraka wa bidhaa ndani na nje ya nchi, zikiwemo mazao ya kilimo kama matunda na mboga mboga, samaki, kuku, maua na bidhaa nyingine zinazohitaji kufikishwa sokoni kwa muda mfupi.

Aidha, amesema uwanja huo utasaidia kuongeza fursa za uwekezaji, utalii, usafirishaji wa mizigo na ajira, huku ukichochea ukuaji wa uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.

DODOMA KUUNGANIKA ZAIDI

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuipa Dodoma, ambayo ni Makao Makuu ya Nchi, uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuhudumia safari za ndani na kimataifa.

Mradi pia unatarajiwa kuboresha huduma kwa wasafiri, wawekezaji na wadau wa sekta ya usafiri wa anga, kuongeza usalama wa safari za ndege na kupunguza changamoto zinazohusishwa na miundombinu iliyopo.

TANROADS inaendelea kufuatilia programu za kazi, upatikanaji na ufungaji wa vifaa, uratibu wa wakandarasi, utekelezaji wa kazi zinazotegemeana pamoja na taratibu za kimkataba ili kuhakikisha tarehe zilizowekwa za kukamilisha mradi zinafikiwa.Maendeleo ya ujenzi wa jengo la abiria.


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta akizungumza na vyombo vya habari uwanjani hapo.



Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari MAELEZO, Zamaradi Kawawa akizunghumza wakati wa kumkaribisha Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta.
Zamaradi Kawawa akijadiliana jambo na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta.



Uwanja wa Msalato unavyoonekna kwa juu

Wanahabari wakiwa katika mkutano huo.



 


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages