Prof. Shemdoe ametoa wito huo leo, Agosti 21, 2026, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), uliofanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 19 hadi 21, 2026, katika Ukumbi wa Jiji Mtumba, jijini Dodoma.
“Niwaase na kuwaomba sana muepuke migogoro miongoni mwenu; kati ya Mkurugenzi na Katibu Tawala, kati ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya, kati ya RAS na Mkuu wa Mkoa, na kati ya kiongozi na watumishi unaowaongoza. Mahali penye migogoro hakuna ufanisi wa kazi na maendeleo,” amesema Prof. Shemdoe.
Amesema viongozi na watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapaswa kufanya kazi kwa kuheshimiana, akisisitiza kuwa hakuna sababu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kupambana na Mwenyekiti wa Halmashauri au Mstahiki Meya.
Prof. Shemdoe amesema uzoefu wake katika uongozi umemfundisha umuhimu wa ushirikiano na kuheshimiana, akieleza kuwa alipokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hakuwahi kugombana na Mwenyekiti wa Halmashauri, na alipokuwa Katibu Tawala wa Mkoa hakuwahi kupishana lugha na Mkuu wa Mkoa.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuidhinisha na kuleta fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Taasisi za Umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema fedha hizo zinaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kujiingizia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), Bw. Albert Gabriel Msovela, amemhakikishia Prof. Shemdoe kuwa wajumbe wa taasisi hiyo ni askari wake kiutendaji na kwamba TOA itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa Katiba.
Bw. Msovela amesema TOA itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza malengo mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Mhe. Waziri, naomba nikuhakikishie kwamba kupitia Mkutano Mkuu huu wa 16 wa Mwaka wa TOA, tutatoka na mikakati, maazimio pamoja na mipango madhubuti ambayo tutakwenda kuwashirikisha wananchi katika utekelezaji wake kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesisitiza Bw. Msovela.
Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa TOA uliowakutanisha Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Makatibu Tawala wa Wilaya, umefanyika chini ya Kaulimbiu isemayo: “Ugatuzi wa Madaraka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Nguzo Madhubuti ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”











No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇