LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 21, 2026

PPRA YANUFAISHA ZAIDI YA MAKUNDI 27,900 KUPITIA MFUMO WA NeST


Na Richard Mwaikenda, Dodoma,

Jumla ya makundi maalumu 27,946 yamesajiliwa katika Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST) na tayari yamefanikiwa kupata zabuni zenye thamani ya jumla ya Shilingi bilioni 56, katika hatua inayolenga kuwawezesha Watanzania wengi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi kupitia ununuzi wa umma.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema hayo leo, Agosti 20, 2026, wakati akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, Mji wa Serikali wa Mtumba, jijini Dodoma.

Simba amesema kati ya makundi hayo, 13,317 ni ya vijana, 13,400 wanawake, 643 wazee na 586 ya watu wenye ulemavu, huku akieleza kuwa usajili huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha fursa za zabuni za umma zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan wale ambao hawana uwezo wa kuanzisha kampuni binafsi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, taasisi zote za umma zinatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalumu, ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

LENGO NI MAKUNDI 300,000

Mkurugenzi huyo amesema PPRA inalenga kuongeza idadi hiyo hadi kufikia takribani makundi 300,000 yaliyo tayari kushiriki katika kuomba na kutekeleza zabuni za Serikali, hatua inayolenga kuunga mkono utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema hatua hiyo inaweza kuzalisha athari kubwa kiuchumi kupitia ajira na kazi zinazoweza kufikia takribani milioni tatu, kutokana na shughuli zitakazotekelezwa na makundi hayo.

“Tunataka kuwa na takribani makundi 300,000 yaliyo tayari kuomba zabuni. Hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kutoa ajira na kazi kwa Watanzania ambao hawana uwezo wa kuwa na kampuni, lakini wanaweza kujiunga kwenye vikundi na kutekeleza zabuni,” amesema Simba.

Ameongeza kuwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi wengi zaidi kushiriki katika uchumi, kundi maalumu linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Shilingi milioni 500.

MWENGE WA UHURU WAONGEZA HAMASA

Simba amesema Serikali imeifanya ajenda ya kuwawezesha makundi maalumu kushiriki katika ununuzi wa umma kuwa miongoni mwa masuala muhimu yanayosisitizwa kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, jambo ambalo limeongeza hamasa ya usajili wa vikundi na utekelezaji wa zabuni.

Amesema PPRA pia imeanza kushirikiana na Ofisi ya Rais – Wizara ya Maendeleo ya Vijana katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga kwenye vikundi, ambapo wanatarajia kufika katika Halmashauri zote 184 nchini.

WATANZANIA WAHIMIZWA KUJIUNGA

Mkurugenzi huyo amewataka Watanzania kutumia fursa hiyo kwa kuunda vikundi vyenye watu watatu au zaidi, kuvisajili katika Halmashauri zao na baadaye kuvisajili katika Mfumo wa NeST, ambao unatumika kuwezesha upatikanaji wa taarifa na zabuni za ununuzi wa umma.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kujenga uchumi jumuishi, ambao unampa kila Mtanzania nafasi ya kushiriki na kunufaika na shughuli za kiuchumi.

“Tunawasihi Watanzania tuendelee kujiunga kwenye vikundi vya watu watatu na kuendelea, kuvisajili kwenye Halmashauri zao, na kisha wasajili kwenye Mfumo wa NeST ambao ndio wenye zabuni zote za umma,” amesema.

Amesema ushiriki mpana wa makundi hayo katika zabuni za Serikali utasaidia kuongeza kipato, ajira na fursa za biashara, huku ukichochea wananchi kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuanzia katika ngazi ya jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba
Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.


 Viongozi wa PPRA katika picha ya kumbukubu baada ya mkutano kumalizika.




No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages