Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) imeimarisha uwezo wake wa kukabiliana na wadudu na ndege waharibifu wa mazao kwa kuongeza vitendea kazi, ikiwemo ndege maalumu kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya mazao.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, leo Agosti 27, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema mamlaka hiyo kwa sasa ina jumla ya ndege nyuki 21 zinazotumika katika shughuli za udhibiti wa visumbufu vya mimea.
Amesema TPHA pia imeagiza ndege nyuki nyingine 20, hatua ambayo itaongeza uwezo wa mamlaka hiyo kufikia maeneo mbalimbali nchini na kuchukua hatua kwa wakati dhidi ya milipuko ya wadudu na ndege wanaoweza kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao.
Prof. Ndunguru amesema, pamoja na ndege hizo, TPHPA imenunua ndege kubwa yenye uwezo mkubwa zaidi, ambayo itatumika katika shughuli za kudhibiti ndege na wadudu waharibifu wa mazao.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha ulinzi wa mazao na kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha visumbufu vinadhibitiwa kabla havijasababisha hasara kubwa kwa wakulima.
“Tumeendelea kuongeza uwezo wetu wa kukabiliana na visumbufu vya mimea. Kwa sasa tuna ndege 21, nyingine 20 tumeziagiza, na pia tumenunua ndege kubwa yenye uwezo mkubwa kwa ajili ya kudhibiti ndege na wadudu waharibifu wa mazao,” amesema Prof. Ndunguru.
Ongezeko hilo la vifaa linatarajiwa kuimarisha uwezo wa TPHPA katika ufuatiliaji, udhibiti na kukabiliana na milipuko ya visumbufu vinavyoweza kuhatarisha uzalishaji wa chakula na usalama wa chakula nchini.





No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇