LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 30, 2026

KAMONGA AIPONGEZA LUDEWA KUPAISHA MAPATO HADI SH. BIL. 5

Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Mhe. Joseph Kamonga, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kwa hatua kubwa iliyopiga katika ukusanyaji wa mapato, akieleza kuwa ongezeko hilo limeiwezesha Halmashauri kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026.


Mhe. Kamonga ametoa pongezi hizo leo tarehe 29 Agosti 2026 wakati akizungumza katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa lililokuwa likijadili Taarifa ya Ufungaji wa Hesabu za Halmashauri kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni 2026.

Amesema Halmashauri imepiga hatua kubwa kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka takribani Shilingi milioni 800 kwa mwaka hadi kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 5, hatua ambayo amesema ni ishara ya kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na usimamizi wa vyanzo vya mapato.

“Tumepiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapato. Kutoka kukusanya takribani milioni 800 hadi kufikia zaidi ya bilioni 5 ni jambo la kupongezwa, na ongezeko hili limeifanya Halmashauri kuvuka lengo lake la ukusanyaji wa mapato,” amesema Mhe. Kamonga.

Hata hivyo, Mhe. Kamonga amewataka madiwani na uongozi wa Halmashauri kuendelea kuwa wabunifu katika kutafuta na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato, badala ya kutegemea kodi na tozo pekee kama chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri.

Amesisitiza umuhimu wa Halmashauri kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayoweza kuzalisha mapato, pamoja na kutambua na kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika Wilaya ya Ludewa.

Kwa mujibu wa Mhe. Kamonga, Ludewa ina fursa kubwa za kiuchumi zinazoweza kuongeza mapato ya Halmashauri, hususan katika kipindi hiki ambacho miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Maganga Matitu, Liganga na Mchuchuma, inaanza kutekelezwa.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa utakapochangia kuongeza shughuli za kiuchumi na uwekezaji katika Wilaya, Halmashauri inapaswa kuwa tayari kutumia fursa hizo kwa kubuni vyanzo endelevu vya mapato vitakavyoongeza uwezo wake wa kutoa huduma na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.


 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages