Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (MCC), Mary Chatanda amesema mageuzi makubwa ya kimaendeleo yaliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan yamekuwa chachu ya vyuo vikuu vya ndani na nje ya Tanzania kumtunuku Shahada mbalimbali za Heshima za Uzamivu.
Chatanda ametoa kauli hiyo Juni 5, 2026, Jijini Dodoma ikiwa ni siku moja imepita tangu Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RADN University) kumtunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa), Jijini Moscow, Urusi.
"Unajua utendajikazi mzuri wa Rais wetu Dk. Samia unaonekana duniani kote, na wengi wanaridhishwa na juhudi kubwa zinazofanywa ana serikali katika kuchochea maendeleo ya nchi. Rais amefanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo, na ndiyo maana wenzetu wa Urusi wamemtunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima," amesema Chatanda.
Sambamba na hilo, Chatanda amesema katika kila sekta, kuna mabadiliko chanya mengi ambayo yamefanyika ndani ya muda mfupi, ndiyo maana hata mataifa mengine yanatambua kazi nzuri zinazofanyika nchini.
Juni 4, 2026, Chuo Kikuu cha RADN kilimtunuku Rais Dk. Samia Shahada ya Udaktari wa Heshima ikiwa ni njia ya kutambua mchango wake katika mageuzi ya sekta ya elimu, kuimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa ikiwemo sekta ya utalii.
Baada ya kutunukiwa Shahada hiyo, Rais Dk. Samia amesema mafanikio hayo si yake pekee yake bali ni juhudi za pamoja kama nchi.
"Shahada hii haihusu mafanikio yangu binafsi, bali ni utambuzi wa mchango wa Watanzania wote katika maendeleo ya Taifa na ushirikiano wa kimataifa. Napokea kwa upole, kama Rais wa Tanzania, mtoto wa Afrika na rafiki wa Russia. Siipokei kwa ajili yangu, bali kwa ajili ya Watanzania," amesisitiza Rais Dk. Samia.
Rais Dk. Samia yupo nchini Urusi kwa ziara ya kikazi, ikiwa ni juhudi za kuimarisha diplomasia ya uchumi na mataifa mengine ili kukuza maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii nchini.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇