LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 1, 2026

CHAMA CHA WATAALAM WA KINYWA NA MENO (TDA) NA SHIRIKISHO LA AFYA YA KINYWA NA MENO DUNIANI (FDI) WAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA CHUO KIKUU CHA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI (MUHAS)

Chama cha Madaktari wa Meno Tanzania (TDA) na Shirikisho la Madaktari wa Meno Duniani ( FDI) wameahidi kuendeleza uhsirikiano na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika kuendeleza elimu ya tiba ya meno na huduma za afya.

Ahadi ya ushirikiano huo ilifikiwa mwishoni mwa wiki, wakati Mkuu wa Shule Kuu ya Afya ya Kinywa na Meno, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Dkt. Ferdinand Machibya, alipokuwa akizungumza na Rais wa Shirikisho la kinywa na Meno Duniani (FDI), Prof. Nikolai Sharkov, ambaye alitembelea MUHAS akiwa na ujumbe wake kutoka FDI kwa lengo la kuongeza ushirikiano kati ya MUHAS na washirika wa kimataifa katika kuendeleza elimu ya tiba ya meno na huduma za afya.

Ziara hiyo iliwakutanisha wataalamu wa tiba ya meno, wahadhiri, pamoja na wanafunzi kwa ajili ya kujadili fursa za ushirikiano katika mafunzo, utafiti, na kujengeana uwezo ndani ya sekta ya afya ya meno.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Dk. Machibya, alimkaribisha, Prof. Nikolai Sharkov, chuoni hapo. Alieleza kuwa ziara hiyo inaonesha kuongezeka kwa ushirikiano kati ya MUHAS na washirika wa kimataifa katika kuendeleza elimu ya tiba ya meno na huduma za afya.

Dk. Machibya alisema MUHAS inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi kupitia ufundishaji, utafiti, pamoja na huduma za ushauri wa kitaalamu. Aliongeza kuwa Shule ya Tiba ya Meno imekuwa ikivutia wanafunzi wa shahada za uzamili na wataalamu kutoka nchi mbalimbali wanaojiunga na chuo hicho kwa ajili ya mafunzo maalum na kozi fupi za afya.

Katika ziara hiyo, Prof. Sharkov aliipongeza Shule ya Tiba ya Meno ya MUHAS kwa mchango wake katika sayansi ya afya ya kinywa na meno, na kuisifu shule hiyo kwa kuwa Kituo Bora cha Umahiri katika Sayansi ya Afya ya Kinywa na Meno Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Prof. Sharkov pia aliipongeza MUHAS pamoja na Chama cha Madaktari wa Meno Tanzania kwa mchango wao katika kuimarisha huduma za afya ya meno na kuzalisha wataalamu wenye sifa nchini Tanzania.

Aidha, aliwahimiza wanafunzi wa tiba ya meno kuendelea kuwa makini katika masomo yao na kukuza taaluma zao ili waweze kuchangia ipasavyo katika mustakabali wa huduma za afya ya kinywa na meno.

Tukio hilo lilifanyika katika Shule ya Tiba ya Meno MUHAS na kuhudhuriwa na viongozi wa Chama cha Madaktari wa Meno Tanzania, madaktari wa meno wa kanda mbalimbali, wahadhiri wa MUHAS, pamoja na wanafunzi. 


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages