Utangulizi:
Kanisa ni mwili wa Kristo hapa duniani na ni nuru ya ulimwengu (Mathayo 5:14). Katika taifa lolote, Kanisa lina nafasi ya kipekee ya kusimama kama sauti ya matumaini, hekima na upatanisho. Wakati wa changamoto za kijamii, kisiasa au kiuchumi, macho ya wananchi hutazama kwa viongozi wa kiroho ili waongoze kwa busara na kweli.
1. Kanisa ni Mlinzi wa Amani
Biblia inasema: “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:9).
Wajibu wa Kanisa si kuchochea migawanyiko bali kuwa daraja la kuunganisha watu.
Kuhubiri ujumbe wa upendo, uvumilivu na kusameheana.
Kuepuka lugha za uchochezi au ubaguzi madhabahuni.
Kuombea taifa, viongozi wake na wananchi bila upendeleo.
Amani ya nchi huanza katika mioyo ya watu, na mioyo hubadilishwa kupitia Neno la Mungu.
2. Wajibu wa Wachungaji/ Mapadri ni Kuunganisha Wananchi
Mchungaji na Padri ni viongozi wa kondoo, si wa kundi moja tu bali wa jamii nzima inayomzunguka.
Wachungaji wanapaswa:
Kuepuka kuingiza siasa za migawanyiko kanisani.
Kuhubiri umoja wa kitaifa bila kujali itikadi, kabila au dini.
Kuwashauri waumini wao kuheshimu mamlaka na sheria za nchi (Warumi 13:1).
Kuwa mfano wa upendo na hekima katika matamshi yao.
Kanisa linapogawanyika, jamii nayo hugawanyika. Lakini Kanisa likiwa moja, linakuwa nguzo ya umoja wa taifa.
3. Kanisa Kama Daraja la Maridhiano
Katika nyakati za mvutano, Kanisa linaweza:
Kuandaa mikutano ya maombi ya kitaifa.
Kualika viongozi wa makundi tofauti kwa mazungumzo ya amani.
Kusimama kama msuluhishi pale panapokuwa na migogoro.
Kanisa linaaminika na jamii; hivyo likisimama kwa haki na kweli, linaweza kuzuia machafuko na kuimarisha mshikamano.
4. Umoja wa Kitaifa ni Baraka
Taifa lililo na umoja hupata maendeleo ya haraka. Biblia inasema:
“Tazama jinsi ilivyo vema na kupendeza ndugu wakae pamoja kwa umoja” (Zaburi 133:1).
Umoja huleta:
Maendeleo ya kijamii na kiuchumi
Heshima ya taifa kimataifa
Utulivu kwa vizazi vijavyo
Hitimisho
Kanisa lina wajibu wa kulinda amani ya nchi na kuimarisha umoja wa kitaifa. Wachungaji/ Mapadri waunganishe wananchi, wasiwagawe. Madhabahu iwe mahali pa maombi, si pa malumbano; pa upendo, si pa chuki; pa umoja, si pa mgawanyiko.
Amani ya taifa ni wajibu wa kila mmoja, lakini Kanisa lina nafasi ya kipekee ya kuiongoza njia hiyo.
Sophia Mwakagenda
Mbunge Mstaafu na Mjumbe wa UWT Taifa Nyanda za juu kusini.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇