LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 13, 2026

KUTOKA RUBANI WA NDEGE MAREKANI HADI MUOKOTA KENYA

Kutoka rubani wa ndege nchini Marekani hadi muokota makopo nchini Kenya. Hii ni hadithi ya maumivu ya ndugu Samuel Mawato, mkazi wa Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, nchini Kenya.

Samuel hakuwahi kufikiria kwamba siku moja angekuwa muokota makopo. Kwa miaka 15 aliyoshi Marekani, ambako alisomea urubani na baadaye kufanya kazi kwa muda mfupi katika shirika kubwa la ndege la American Airlines, hakuwahi kufikiria kwamba maisha yake yangeishia kuokota makopo.

Kabla ya kwenda Marekani, Samuel alikuwa akifanya kazi kama mhudumu wa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi. Hata hivyo, ndoto yake kubwa ilikuwa kuwa rubani. Kwa jitihada na maombi, hatimaye mwaka 1998 alipata fursa adimu ya ufadhili wa masomo ya urubani nchini Marekani kupitia Kanisa la Methodist.

Alijiunga na chuo mashuhuri cha ATP Flight School kampasi ya Arizona. Kwa miaka miwili alijifunza urubani na kupata leseni ya awali ya kurusha ndege binafsi (Private Pilot License – PPL). Aliendelea na mafunzo na baada ya miaka miwili zaidi akapata leseni ya kurusha ndege za kibiashara (Commercial Pilot License – CPL).

Baadaye alipata kazi kama rubani msaidizi (First Officer) katika shirika la American Airlines. Alioa mwanamke wa kizungu na kuanzisha familia. Walifanikiwa kupata watoto wawili katika ndoa yao: wa kike na wa kiume.

Mambo yalianza kubadilika baada ya Samuel kutaka kurudi Kenya na kutumia ujuzi wake kusaidia taifa lake. Walitofautiana na mkewe ambaye hakuwa tayari kuhamia Kenya. Alimtaka Samuel waendelee kuishi Marekani. Lakini Samuel aliona kubaki Marekani ni usaliti kwa jamii yake na kanisa lililomemomesha.

Mvutano huo ulisababisha ndoa yao kupasuka. Mkewe akabaki Marekani na watoto, Samuel akarudi Kenya. Baada ya miaka 15 ya kukaa ughaibuni, Samuel aliamini kurejea kwake Kenya kungekuwa mwanzo wa maisha bora na yenye matumaini. Alipoingia Kenya, akaoa mke mwingine.

Hata hivyo, mambo hayakuwa kama alivyotarajia. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya (KCAA), rubani aliye somea nje ya nchi hutakiwa kufanya refresher training na kutimiza angalau 200 flight hours ili leseni yake itambulike na kuruhusiwa kurusha ndege kibiashara. Samuel alikuwa ameanza kupungukiwa na fedha, hivyo akachukua mkopo kuweka gari yake rehani ili apate fedha za kushiriki mafunzo hayo.

Fedha alizopata hazikutosha kulipia masaa yaliyohitajika. Zikaisha kabla hajamaliza mafunzo. Benki aliyokopa ikataifisha gari yake baada ya kushindwa kufanya marejesho. Hivyo akapoteza gari na mafunzo hakumaliza. Akiwa katika mtanziko, mkewe (yule aliyemuoa Kenya) akamtoroka.

Maisha yakaanza kuwa magumu. Miaka 15 aliyokuwa Marekani ilitosha kumpotezea baadhi ya marafiki na jamaa. Aliporudi, hawakuwa tena karibu naye kama zamani. Alipojaribu kuwaomba msaada, wengi walimkwepa. Hapo ndipo maisha yakazidi kuwa magumu kwake.

Hatimaye ikamlazimu kufanya kazi yoyote ili mradi mkono uende kinywani. Alianza kwa kuendesha toroli, lakini kadri umri ulivyosonga ndivyo nguvu zilivyomuishia. Hatimaye akaamua kujikita katika shughuli ya kuokota makopo. Na sasa ameanzisha kikundi kiitwacho Responsible Citizen Initiatives kwa ajili ya kuhamasisha usafi wa mazingira Kilifi.

Leo akiwa na umri wa miaka 64, Samuel anajikongoja taratibu mitaa ya Mtwapa huko Kilifi akiokota makopo kama shughuli pekee inayoendesha maisha yake. Bado anakumbuka jinsi alivokuwa na imani kwamba uzoefu wake wa ng’ambo ungefungua milango baada ya kurejea nyumbani. Lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia.

Hana mawasiliano na mkewe wa Marekani wala watoto wao wawili kwa miaka mingi sasa. Anajua kwamba wanae kwa sasa ni watu wazima na huenda hata akikutana nao wasimtambue, lakini hajakata tamaa.

Katika umri wa uzee, mwili kudhoofu na maisha ya upweke, bado Samuel analo tumaini. Anaamini siku moja Mungu atampa nafasi ya kukutana na watoto wake, walau awaone tu na kuwakumbatia kabla hajafa. Hilo ndilo ombi lake kubwa kwa sasa.

Je nini maoni yako? Samuel alikosea kurudi Kenya? Samuel hakujipa muda wa kupata taarifa sahihi kabla ya kurudi? Watu wenye vipawa vikubwa na akili nyingi wameshindwa kustawi Afrika kutikana na mifumo mibovu?







 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages