Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amemtaka Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Ngilangwa, kuipa majibu klabu ya Simba SC kuhusu mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji (transformation), akisisitiza kuwa kabla ya mwezi huu kumalizika jambo hilo liwe limekamilika.
Makonda amesema katika kipindi cha uongozi wake sheria na kanuni zitafuatwa kikamilifu, na kwamba lengo ni kuona timu zinafanya vizuri bila sintofahamu za kiuongozi kuathiri maendeleo yao.
Kauli hiyo ya Waziri Makonda inakuja wakati mjadala ukiendelea miongoni mwa mashabiki na wadau wa Simba kuhusu hatma ya mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo. Hivi karibuni, Mwekezaji na Rais wa heshima wa klabu ya Mohammed Dewji aliibua mjadala baada ya kuandika kwenye uwanja wa maoni kwenye ukurasa rasmi wa Simba akiuliza, “Transformation mmefikia wapi?”
Swali hilo lilikuja kufuatia maelezo ya Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, kuhusu taratibu za kadi mpya za kisasa kwa wanachama, jambo lililochochea mashabiki wengi kutaka ufafanuzi zaidi juu ya mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu.
Sasa macho ya Wanasimba yanaelekezwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo kusubiri majibu rasmi kabla ya mwezi huu kumalizika, kama alivyoelekeza Waziri Makonda.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇