Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali yake ya Awamu ya Sita imeandika historia nyingine kubwa kwa Taifa kwa kuzindua Makao Makuu ya kwanza ya Ulinzi wa Taifa mkoani Dodoma na kwamba hatua hiyo imekamilisha maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1964 wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilipoundwa.
"Leo tumeandika historia nyingine kubwa kwa Taifa letu kwa kuzindua Makao Makuu ya kwanza ya Ulinzi wa Taifa eneo la Kikombo mkoani Dodoma. Hatua hii imekamilisha maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1964 wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilipoundwa."
"Majengo haya ambayo tumeyajenga kwa fedha na wataalamu wa ndani ni uthibitisho wa ukomavu wa Taifa letu katika kupanga, kuamua na kutekeleza kwa ufanisi miradi mikubwa. Kuziweka pamoja ofisi za JWTZ na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kutaongeza tija na ufanisi wa kazi, na ni kielelezo cha dhamira yetu ya kujenga taasisi imara za kulinda uhuru, mipaka, rasilimali na watu wetu," amesema Rais Samia huku akishangiliwa.
"Mafanikio ya mipango tuliyojiwekea yanategemea sana uwepo wa amani na utulivu. Hivyo, wito wangu kwetu sote ni kuendelea kuimarisha ulinzi, usalama, umoja na mshikamano wa nchi yetu." Amesema Rais Samia.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa JKT ,Dkt .Rhimo Nyansaho amesema ujenzi wa makao makuu hayo unaonesha dhamira ya wazi ya serikali katika kuimarisha suala la ulinzi na usalama nchini.
Amesema jengo hilo la kisasa litaongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za kiulinzi na kutoa mazingira bora ya utendaji kazi kwa maafisa na askari.
“Uwepo wa makao makuu ya kudumu ni hatua muhimu katika kujenga taasisi imara, zenye mifumo madhubuti ya kiutendaji na mawasiliano, jambo litakalosaidia kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazoibuka katika ulimwengu wa sasa.”amesema Dkt.Nyansaho.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe amesema serikali imeandika historia mpya kwa kuwa na makao makuu ya kudumu ya ulinzi wa taifa.
Amesema zaidi ya shilingi bilioni 121 zimetumika katika kufanikisha ujenzi huo wa awamu ya kwanza ambao umetekelezwa na wataalamu wa ndani ya jeshi hilo.
“Matumizi ya wataalamu wa ndani yamepunguza gharama na kuongeza uzoefu kwa wanajeshi katika sekta ya ujenzi na usimamizi wa miradi mikubwa ya kimkakati. ameongeza kuwa mradi huo umezingatia viwango vya kisasa vya ubora na usalama.”amesema Dkt.Mnyepe.
Kwa upande wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda amesema jengo hilo ni sehemu ya kurahisisha utendaji kazi na kuchochea uimarikaji wa ulinzi na usalama wa taifa. amesema makao makuu hayo yatawezesha upangaji na utekelezaji wa mikakati ya kiulinzi kufanyika kwa haraka na ufanisi zaidi.
Aidha amewahimiza wanajeshi kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu na uzalendo, wakitambua kuwa jukumu lao ni kulinda uhuru, umoja na mshikamano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇