NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
WAKATI Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikiitunukia Cheti cha Shukrani na Pongezi kwa kufadhili, kudhamini na kushiriki Siku ya Kitaifa ya Mazoezi, Benki ya NMB imetambia ushinriki na udhamini wake katika matukio mbalimbali yanayoambatana na Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
NMB imepokea cheti hicho kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, baada ya kumalizika kwa matembezi maalum yaliyoanzia Viwanja vya Mapinduzi Square Michezani hadi Uwanja wa New Amaan, yalikofanyika mazoezi ya viungo ya pamoja.
Katika kufanikisha matembezi na mazoezi hayo yaliyoshirikisha zaidi ya watu 6,000 kutoka vikundi zaidi ya 170 vya mazoezi Tanzania Bara na Zanzibar, NMB ilikabidhi ‘tracksuit’ 100 za kuvaa viongozi waandamizi wa SMZ wakiongozwa na Rais. Dk. Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla.
Akihutubia washiriki wa mazoezi hayo, Dk. Mwinyi aliwapongeza wadhamini wote waliofanikisha kufana kwa Siku ya Kitaifa ya Mazoezi na kwamba mchango wao katika siku hiyo muhimu kwa ustawi wa afya za Wazanzibar una thamani kubwa, huku akiwataka washiriki kudumisha utamaduni huo.
“Nawashukuru wadau na wafadhili wote, waliotoa michango yao katika kufanikisha bonanza hili linaloandaliwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa Kushirikiana na Chama cha Mchezo wa Mazoezi Zanzibar (ZABESA).
“Mazoezi ya viungo ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu kwani yanachangia kuimarisha afya ya mwili na akili na kukinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
“Bonanza hili ni jukwaa muhimu la kuwakumbusha wananchi kuwa afya njema ni nyezo muhimu ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Nitumie fursa hii kusisitiza ushiriki wa michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kikapu, wavu, riadha na michezo ya majini,” alisema. Dk Mwinyi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed Nassor, alisema benki yake inajivunia sio tu ufadhili na ushiriki wa Siku ya Kitaifa ya Mazoezi, bali udhamini na mchango wao wa jumla katika Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Nassor ambaye pia ni Meneja wa NMB Tawi la Mwanakwerekwe, alisema kwa miaka 13 sasa benki yake imekuwa ikishiriki matukio mbalimbali ambayo yanakuwa sehemu ya shamrashamara za Maadhimisho ya Mpinduzi, ikiwamo mwaka huu waliodhamini mashindano ya soka ya Kombe la Mapinduzi.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutambua mchango wetu na kutupatia cheti cha shukrani kwa ufadhili wetu wa kufanikisha bonanza hili, lakini pia sisi kama benki tunajivunia mchango wetu wa jumla katika matukio yanayoambatana na sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
“Tumetoa ‘tracksuit’ 100 za kuvaa viongozi wa SMZ katika bonanza hili, lakini pia tumekuwa wadhamini wakuu wa NMB Mapinduzi Cup – mashindano ya soka yanayoendana na sherehe hizi za Mapinduzi. Tumekuwa tukifanya hivi kila mwaka kusapoti na kushiriki matukio yote yanayoambatana na sherehe hizi.
“Sisi kama benki tunayojali na kuthamini afya, tumekuwa tukichangia misaada ya kufanikisha, zaidi ya yote tunashiriki pia kama mlivyoona leo. Tunajivunia hilo na tunaahidi kushirikiana na SMZ katika kushajihisha shamrashamra za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo yanatimiza miaka 62 mwaka huu,” alisema Nassor.





No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇