Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo, amelaani tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kutumia mamlaka na ushawishi wao kwa waumini kuhalalisha migogoro na migawanyiko ndani ya mataifa yao.
Leo, ambaye ni Papa wa kwanza kutoka nchini Marekani, ameyasema hayo kupitia ujumbe wa kurasa nne uliotolewa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani ya Kanisa Katoliki, yanayolenga kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha, na kudumisha amani katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 18, 2025, Papa Leo amesema kumekuwa na baadhi ya viongozi wa dini wanaotumia kigezo cha sera za uzalendo, kama nyenzo ya kupandikiza chuki miongoni mwa waumini kitendo ambacho amekiita ni kufuru, au dhambi kubwa inayomdharau na kumtukana Mungu.
"Kwa bahati mbaya, imekuwa jambo la kawaida zaidi kuivuta lugha ya imani katika vita vya kisiasa, kubariki utaifa, na kuhalalisha vurugu na mapambano ya silaha kwa jina la dini," amesema Papa.
Amesema waumini lazima wajue kukanusha kikamilifu, mafundisho na maelekezo yote ya viongozi wa dini ambao wamekuwa na tabia hii, ili kuondoa uwezekano wa kutokea kwa migogoro ndani ya Taifa.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇