LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 30, 2025

NAULI YA UHALIFU SGR INAUMIZA, INAFURAHISHA

 KUNA Jambo moja ambalo baadhi ya abiria wanaosafiri kwa Treni ya SGR hawalifahamu au wamekumbana nalo, ambalo lina maumivu kwao,lakini linalinufaisha Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kuchangia pato la Taifa.


‎Jambo hilo ni Nauli ya Uhalifu ambayo ni faini anayotozwa mara mbili ya nauli anakokwenda abiria anayekutwa ndani ya treni bila kuwa na tiketi.


‎Adhabu hiyo humkumba pia mtu yeyote mwenye shida ya kusafiri  baada ya kukosa tiketi, lakini akawaomba wahusika kwa kuwaeleza umuhimu wa kuwahi kufika anakokwenda.


‎Mimi ambaye ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa usafiri huo, nimekuwa mara kwa mara nikishuhudia utozwaji wa faini hiyo ya Uhalifu ambayo ni dhahiri inawaumiza abiria hao.


‎Kinachonifurahisha ni pale ninapoona wahudumu wa SGR wakitumia mashine maalumu kuwakatia tiketi halali, Jambo linaloniaminisha kuwa malipo yaliyofanyika hayaendi mifukoni mwao, bali yanaingia Serikalini.


‎Siku moja nikisafiri kutoka Dodoma kwenda Dar, nilishuhudia abiria mmoja mwanaume aliyepandia Gulwe kwenda Morogoro akiwa na mtoto wa kike wa umri wa miaka 6, ambaye hakuwa na tiketi, akilipishwa faini hiyo.


‎ Abiria aliambiwa kuwa sheria SGR hairuhusu mtoto wa umri huo kusafiri bure, bali anayeruhusiwa ni mtoto chini ya miaka minne na kwamba zaidi ya umri huo yapaswa alipe nusu nauli na kupatiwa kiti.


‎Ndipo kwa shingo upande alilipa faini hiyo na kupatiwa tiketi. Likaja zogo lingine la kumtenganisha yeye na mtoto ambaye alitafutiwa kiti mbali na yeye, Jambo ambalo hakukubaliana nao kwani yeye alitaka ampakate Ili awe pkaribu naye kwa uangalizi wake, lakini alikataliwa kwa kuelezwa kuwa sheria haziruhusu.



‎Adhabu nyingine anayokumbana nayo abiria huyo mhalifu' ni kukosa kiti hadi kitakapoachwa wazi na abiria mwingine atayeshuka kituo cha jirani.


‎Licha ya kulipishwa faini hiyo, wahudumu wamekuwa wakionekana kuwa wakali na hawapendezwi na tabia hiyo ya abiria kukutwa kwenye treni bila tiketi, kwani sheria za SGR haziruhusu, lakini pia haitakiwi abiria kusafiri bila kuwa na kiti.


‎Akielezea hatua zaidi zinazochuliwa kwa abiria anayepanda treni ya SGR na kukaidi kulipa faini hiyo ya uhalifu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Fred Mwanjala amesema kuwa;


‎Kwa mujibu wa kifungu namba 10 cha Sheria ya uendeshani wa TRC ya Mwaka 2017 ni kwamba ni marufuku abiria yeyote kupanda treni bila tiketi au kukutwa na tiketi feki na akibainika atalipishwa faini na endapo atakaidi atakamatwa na kukabidhiwa kwa Askari Polisi wa Kitengo cha Reli ambao wamo ndani ya Treni.


‎Amesema kwa kuwa kosa hilo ni la kijinai, mtuhumiwa atapelekwa Mahakamani  kwa hatua zaidi za kisheria.


‎IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA - 0754264203


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages