Gridi ya Taifa ya Maji ni Mkakati wa Taifa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika kuhakikisha kunakuwa na huduma endelevu ya maji kwa jamii, viwanda, kilimo, mifugo na mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wasilisho hilo, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema
mpango huo wa gridi ya taifa ya maji utasaidia kutatua changamoto kwa kuwa na vyanzo vya uhakika vya Maji kutoka Maziwa Makuu na mito mikubwa.
Amebainisha kuwa Tanzania ni kinara wa ajenda ya maji Afrika kupitia uwekezaji wa miradi mikubwa ya maji ambayo inatekelezwa na Serikali ili kukabiliana na uhaba wa huduma hiyo muhimu kwa binadamu.
Akiendelea kuzungumza, Bw. Mitawi alisema kuwa pamoja na mambo mbalimbali gridi ya taifa ya maji itasaidia katika kuwezesha ukuaji wa uchumi na huduma za maji kuwa endelevu na uhakika.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mitawi alisema kuwa Serikali itaendelea kuwashirikisha washirika wa maendeleo kutoka sekta binafsi na asasi za kiraia kuhakikisha maandalizi ya gridi ya taifa ya maji yanachukua nafasi yake na kukamilisha mpango huo muhimu.
Kwa mantiki hiyo alisema kuwa ni wajibu wa kila mmoja ni kulinda vyanzo vya maji yakiwemo maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyka pamoja na mito ili kuhakikisha usalama wa maji unakuwa endelevu kwa wakati wote.
Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru washirika wa maendeleo kama Shirika la kimataifa la WaterAid, NDC Partners na Shrika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) kwa kushiriki katika jitihada za Serikali za kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania Bi. Manka Mushi alisema shirika hilo gridi ya taifa ya maji inaakisi mikakati ya Serikali ya kutatua changamoto ya upungufu wa maji.
Hivyo, alibainisha kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika si tu unatatua changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo wa uhakika bali sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, uvuvi, nishati, viwanda, afya na elimu.
Bi. Manka alipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kuja na mpango wa kuamzisha gridi ya taifa ya maji ambayo itatatua changamoto ya uhaba wa upatikanaji wa huduma hiyo.
Itakumbukwa kuwa Machi 22, 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza ianzishwe Gridi ya Taifa Maji ili maji yaweze kufika katika maeneo yote nchini.Aidha, wakati akifungua Bunge la 13 amesisitiza utekelezaji wa Gridi ya Maji ya Taifa kukamilika ifikapo Mwaka 2030.


No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇